Ubomoaji huu unatokana na wasiwasi kuwa kuwasili kwa kimbunga Elsa kunaweza kukasababisha kubomoka kwa upande wa pili, na upo uwezekano wa kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wanaofanya shughuli za uokoaji.
Msaidizi Mkuu wa kitengo cha Zima Moto cha Miami-Dade, Raide Jadallah amewaambia wanafamilia wa watu 121 waliokuwa hawajapatikana kuwa shughuli za uokoaji zimesimama Jumamosi mchana, habari ambazo mmoja wa ndugu za watu waliokuwa hawajapatikana amesema “zimewaumiza.”
Wafanyakazi wanaovunja jengo wameanza kutoboa matundu kuweka vilipuzi katika zege la jengo la ghorofa 12 la Champlain Towers South upande wa Surfside. Jadallah amesema ubomoaji huo hautafanyika mpaka Jumatatu, ikiwa ndiyo mapema zaidi.
“Iwapo jengo litabomolewa, itakuwa ni salama kwa timu za waokoaji na watafutaji, kwa sababu hatujui lini upande uliobakia utaanguka,” Gavana wa Florida Ron DeSantis amesema mapema Jumamosi katika mkutano na waandishi wa habari, akielezea hatari za mabaki ya jengo hilo lililoanguka.
Maafisa Jumamosi wamesema idadi ya vifo kutokana na kuporomoka kwa jengo hilo Juni 24 iliongezeka kufikia vifo 24 nyakati za usiku, na hadi sasa watu 124 hawajapatikana.
Chanzo cha Habari : VOA News