Waganda wapiga kura katika uchaguzi ulokua na ushindani mkubwa

Wagombea urais Yoweri Museveni (kushoto) na Robert Kyabulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Waganda wanapiga kura Alhamisi katika uchaguzi wa rais unao wapambanisha kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni na upinzani uliopewa nguvu na mwimbaji maarufu Bobi Wine licha ya kampeni ambazo zimetawaliwa na ukandamizaji mkali.

Upigaji kura ulianza kwa kuchelewa kati ya dakika 60 hadi 90 kwenye vituo sita vya kupigia kura ambavyo vilitembelewa na Reuters baada ya karatasi za kura kutofika kwa wakati. Mistari ya wapiga kura ilikuwa ikiongezeka katika vituo vingi wakati wa mchana ulipokaribia na polisi na wanajeshi wakiwa wamevalia vifaa vya kutuliza ghasia walifanya doria katika mji mkuu.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye karibu watu milioni 46 ilikuwa imezimiwa mitandao baada ya mdhibiti wa mawasiliano kuwaamuru waendeshaji wa kampuni za simu kusitisha huduma kuanzia Jumatano, kulingana na mwendeshaji mkubwa nchini Uganda, kampuni ya mawasiliano ya Afrika Kusini ya MTN Group.

Msanii wa Reggae Bobi Wine, 38, anawakilisha hasira za vijana wengi wa Uganda ambao wanasema kiongozi wa zamani wa uasi Museveni, ambaye sasa ana miaka 76, ni dikteta asiyefahamu yanayojiri na aliyeshindwa kushughulikia ukosefu wa ajira na kuongezeka kwa deni la taifa.