Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:05

Wanasiasa wa Upinzani Uganda waahidi kushirikiana kuzuia wizi wa kura na baada ya uchaguzi


Robert Kyagulanyi akiwa na Dr. Kiiza Besigye
Robert Kyagulanyi akiwa na Dr. Kiiza Besigye

Vyama tofauti vya upinzani na wadau mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika alhamisi wiki ijayo, wamekubaliana kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu katika hesabu ya kura.

Wamekubaliana pia kushinikiza jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuchunguza kile wanataja kama ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu nchini Uganda unaofanywa na serikali Pamoja na wanajeshi.

Wanasaisa na wanaharakati hao wakiongozwa na wanasiasa wa mda mrefu Paul Ssemogerere, Dr. Kiiza Besigye, miongoni mwa wengine wametangaza kile wametaja kama makubaliano muhimu yatakayobadilisha siasa za Uganda hata baada ya uchaguzi mkuu.

Mengi katika makubaliano hayo yamebaki siri kati ya wahusika, lakini yanayojulikana kwa waandishi wa habari ni kwamba wamekubaliana kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu utafanyika katika hesabu ya kura, katika uchaguzi wa wiki ijayo, Alhamisi Januari 14.

Wamekubaliana kwamba wanasiasa wa upinzani wote watashirikiana kwa karibu san ahata baada ya uchaguzi mkuu, japo lengo la ushirikiano huo halijawekwa wazi, na hawajaeleza ni kwa nini hawawezi kushirikiana sasa na kuwa na mgombea mmoja kati yao kukabiliana na rais Yoweri Museveni, lakini washirikiane baada ya mshindi na aliyeshindwa kujulikana.

Wycliffe Bakandonda ni kiongozi wa muungano huo.

“Lengo letu kubwa ni kulinda kura na kuhakikisha kwamba matokeo yanayotangazwa ni ya kweli. Tumekubaliana kushirikiana na kufanikisha hilo.”

Iwapo mmoja wa wagombea wa upinzani atashinda kiti cha urais na kumuondoa rais Yoweri Museveni, vigogo hao wa upinzani wamekubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Makubaliano haya, yanatoa picha kwa kiasi fulani, sababu kwamba wagombea wote wa upinzani 10, hawajakuwa wakishambuliana kwa maneno katika kampeni, na iwapo mmoja wao amekuwa akikamatwa na kuzuiliwa na polisi, wote wamekuwa wakisitisha kampeni zao na kutaka mwenzao kuachiliwa huru.

Dr. Kiiza Besigye, ameonya kwamba ili malengo hayo yafanikiwe, juhudi zinahitajika kutoka kwa kila mmoja.

“Kama kweli tunataka kuona mabadiliko tunayotaka, tunastahili kufanya mengi zaidi ya tunayofanya usiku na mchana kwa sababu hatuna mda kabisa.” Amesema Besigye.

Wanasiasa na wanaharakati hao wamekosoa hatua ya rais Yoweri Museveni kutumia wanajeshi katika uchaguzi mkuu kama ngao dhidi ya wapinzani wake kisiasa.

Paul Semogerere, amesema kwamba hakuna vile wanajeshi wanaweza kuhusika katika uchaguzi kwa njia ya utulivu na amani kwa sababu mafunzo wanayopokea ni ya kulinda nchi dhidi ya adui na lugha wanayoelewa ni kutumia nguvu dhidi ya adui na wala sio kushirikiana na raia.

“Tafadhali achana na wanajeshi wafanye kazi yao ya kulinda nchi dhidi ya maadui kutoka nje. Wanajeshi hawastahili kutumika katika kusimamia uchaguzi. Usiwape wanajeshi mzigo wa kufuata maslahi ya kisiasa ya walio madarakani wala kuwa kinga kwa rais Museveni dhidi ya wapinzani wa kisiasa ambao hata hawana silaha.”

Katika uchaguzi wa mwaka 2016, chama kikubwa cha upinzani cha Forum for democratic change -FDC, kilikuwa na mpango kama huo wa kuhakikisha kwamba hakuna wizi wa kura unafanyika. Chama hicho kiliunda kituo chake cha kuhesabu kura lakini wasimamizi wote wa chama walikamatwa, ofisi kuzingirwa na polisi na msako mkali kufanyika. Dkt Kiiza Besigye aliyedai kuibiwa kura, alikamatwa na kusafirishwa kwa ndege ya polisi hadi Moroto, karibu kilomita 500 kutoka Kampala.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG