Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 03:55

Museveni ateua wanajeshi kusimamia usalama Kampala wakati wa uchaguzi


Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Wapiga kura, wanasiasa wa upinzani na wachambuzi wa maswala ya usalama nchini Uganda, wana wasiwasi mkubwa kufuatia hatua ya rais Yoweri Museveni kuteua wanajeshi kusimamia usalama wakati wa kipindi hiki cha uchaguzi.

Museveni, ambaye amewataja polisi kuwa wazembe na watu ambao wameshindwa na kazi, ameweka jiji la Kampala chini ya makamanda wa jeshi ambao wamekuwa Somalia na Sudan kusini wakipambana na waasi na makundi ya wapiganaji.

Hatua ya rais Yoweri Museveni kuteua makamanda wa jeshi kufanya kazi ya polisi kabla, wakati na baada ya uchaguzi, imejiri mwezi mmoja baada ya kutokea maandamano yaliyopelekea vifo vya watu 57 baada ya kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

Akitishia kila mara kwamba wale wanaotaka kutatiza usalama wa nchi, kuwatishia wafuasi wa chama chake cha National resistance movement NRM, au kuandamana watakabiliwa kwa nguvu zote, Museveni amesema kwamba jeshi la polisi limeshindwa na kazi akiongezea kwamba polisi wamejaa vidudu.

Mwanajeshi ateuliwa kuwa naibu wa mkuu wa polisi

Baada ya kumfuta naibu wa polisi Maj Gen Sabiiti Muzeyi, Museveni ameteua makamanda kadhaa wa jeshi wanaojulikana kwa kutumia nguvu, kusimamia usalama wa Kampala, Pamoja na wilaya zilizo karibu. Museveni hajawahi kushinda kura katika eneo la Kampala na sehemu zilizo karibu tangu aingine madarakani.

Naibu wa msemaji wa polisi Maj Gen Paul Lokech ametetea uteuzi huo.

“usalama unahitaji ushirikiano. Tusidhani kwamba ni jukumu la polisi pekee kushughulikia usalama. Tunahitaji ushirikiano na polisi. Hawa wanajeshi hawawezi hata kuua nzi.” Amesema MajGen Lokech amesema.

Miongoni mwa wanajeshi walioteuliwa ni Maj Gen. Paul Lokech ambaye kabla uteuzi huo, alikuwa akipambana na waasi nchini Sudan kusini, Maj Gen Kayanja Muhanga ambaye sasa anaongoza shughuli zote za uslama jijini Kampala. Kayanja alikuwa kamanda wa jeshi la Amisom nchini Somalia akipambana na kundi la Al-shabaab. Wengine ni Maj Gen Sam Kawagga, Maj Gen Leopold Kyanda, Maj Gen Abel Kandiho na Brig Gen CS Ddamulira. Makamanda wote wanapokea masharti kutoka kwa rais Yoweri Museveni.

Wanasiasa wa upinzani wanadai uteuzi huo ni wa kuwatisha wapiga kura

Wanasiasa wa upinzani na wachambuzi wa usalama, wanasema uteuzi huu ni ishara ya kuwatisha wapiga kura na kuzima maandamano yanayoweza kujitokeza baada ya uchaguzi mkuu kulalamikia matokeo.

Asuman Basalirwa ni wakili nchini Uganda.

“Tayari kuna watu wana uoga mwingi sana wa kwenda kupiga kura. Kila mahali unapita, unaona wanajeshi. Wanahisi kwamba hawa wanajeshi wanaweza kuwapiga risasi na kuwaua. Wanajeshi wetu ni wakali sana, tunaona mambo yakiwa mabaya sana.”

Kulingana na Basalirwa, idadi kubwa ya wanajeshi wanaoshika doria, ni ujumbe kwa wapiga kura.

“Kwamba yeye ni amri mkuu wa jeshi. Yeye hawezi kuondoka madarakani hata msipompigia kura kwa sababu wanajeshi watamlinda na kumuweka madarakani.”

Wagombea wa urais wakamatwa

Wakati huo huo, wanasiasa wa upinzani wanaendelea kukamatwa, kwa kile polisi wanasema kwamba ni kukiuka maagizo ya tume ya uchaguzi, kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Mgombea wa urais kupitia chama cha FDC Patrick Amuriat, amekamatwa hii leo (Jumanne Januari 5 2021) akijaribu kuingia wilayani Kasese kufanya kampeni.

Tume ya uchaguzi ilipiga marufuku shughuli za kampeni katika wilaya 12 ikisema kwamba maambukizi yameenea katika wilaya hizo. Lakini wachambuzi wa siasa Uganda wanasema wilaya ambazo kampeni zimepigwa marufuku ni ngome ya wanasiasa wa upinzani hasa Robert Kyagulanyi.

Uchaguzi wa Uganda utafanyika wiki ijayo Alhamisi Januari 14 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG