Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:10

Waliopigwa risasi na kuuawa Uganda wana umri kati ya miaka 14 na 30


Idadi kubwa ya watu waliopigwa risasi wakati wa maandamano yaliyotokea Uganda mnano mwezi Novemba mwaka uliopita 2020 baada ya kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, walikuwa na umri kati ya miaka 14 na 30.

Karibu watu wote waliouawa walipigwa risasi na maafisa wa uslama kichwani, kwa shingo, mbavuni, tumboni, kifua na mgongoni.

Kati ya waliouawa pia ni mlinda usalama wa mtaani aliyekuwa ameajiriwa katika mpango mpya wa serikali yar ais Museveni kuwajiri vijana na kuwapa mafunzo namna ya kusaidia maafisa wa polisi kuimarisha usalama nchini Uganda.

Kijana huyo alipigwa risasi na kamanda wa jeshi aliyemwamurisha kumpiga risasi mtu aliyekuwa akiandamana lakini akakataa kwa sababu alikuwa anamjua mtu ambaye alikuwa ameamurishwa kumuua.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, maafisa wa usalama waliokuwa wamevalia sare za jeshi la Uganda UPDF waliwapiga risasi na kuwaua waandamanaji hao.

Mauaji mengine yalifanywa na maafisa wa usalama ambao hawakuwa wamevalia sare za kazi lakini walijaa mjini Kampala na miji ya karibu kuzima maandamanoo hayo ya siku mbili.

Idadi kubwa ya waliouawa hawakuwa wakiandamana

Gazeti la Daily monitor linaripoti kwamba karibu nusu ya darzeni ya waliouawa katika maandamano hayo walikuwa wanafunzi, 11 waendesha pikipiki maarufu kama boda boda na sita watengenezaji wa magari.

Watu wengine kadhaa wanauguza majeraha ya risasi katika hospitali mbalimbali nchini Uganda.

Wengi wa waliouawa pia walikuwa wamesimama kando mwa barabara wakati polisi walikuwa wanawatawanya waandamanaji, na hivyo kupigwa risasi kwa mazingira tatanishi.

Maafisa wa usalama wanasema wanaendela na uchunguzi

Kufikia sasa, jeshi la Uganda limesema kwamba linaendelea na uchunguzi kutambua waliohusika na mauaji hayo, bila kukubali kwamba wanajeshi wake wala maafisa wa polisi walihusika.

Msemaji wa idhara ya uchunguzi wa kihalifu katika jeshi la polisi la Uganda Charles Twine, ameambia gazeti la Daily monitor kwamba “uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo unaendelea lakini sio kila tukio katika upigaji risasi kiholela ni tukio la kihalifu.”

Karibu watu 30 waliuawa jijini Kampala na wengine zaidi ya 25 kuuawa katika miji iliyo karibu na Kampala, ya Mukono, Masaka, Luweero, Jinja, Kyotera na Rakai.

Miji sita ambapo watu wengi waliuawa inapatikana eneo la Uganda lenye jamii ya Baganda, anakotola mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

Maandamano yalitokea Novemba 18 baada ya polisi kumkamata Bobi Wine akiwa katika kampeni wilayani Luuka, mashariki mwa Uganda. Polisi walidai kwamba Bobi Wine alikuwa amekataa kufuata maagizo ya maafisa wa tume ya uchaguzi katika kampeni kwa kuhutubia umati mkubwa wa wat una hivyo kuhatarisha jamii kwa kusambaza virusi vya Corona.

Museveni adai waandamanaji wanafadhiliwa

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa akilaumu wanasiasa wa upinzani kwa maandamano yaliyopelekea mauaji hayo.

Amedai kila mara kwamba wanasiasa wa upinzani wanashirikiana na watu ambao hajawataja, akiesmea wanalenga kuangusha utawala wake kupitia fujo na vurugu.

Amedaiwatu hao wapo nchi za magharibi.

“Tumekuwa tukiwafuatilia kupitia kwa mbinu zenu za ujausi. Wanashirikiana na makundi ya uhalifu ambayo yanawalipa pesa na kuwapa madawa ya kulevya ili kufanya uhalifu katika baadhi ya sehemu za Kampala,” amedai Museveni.

Museveni ateua wanajeshi kudhibithi Kampala

Rais Museveni alimfuta kazi naibu wa mkuu wa Polisi Maj Gen. Muzeyi Sabiiti na kumteua maj. Gen. Paul Lokech anayejulikana kuwa generali mwenye mbinu kali za kukabliana na uhalifu na ambaye ameongoza oparesheni za kiusalama dhidi ya waasi nchini Sudan kusini.

Museveni pia amemteua Maj Gen Kayanja Muhanga kuwa msimamizi wa shughuli zote za usalama jijini Kampala. Atakuwa anapokea masharti moja kwa moja kutoka kwa rais Yoweri Museveni.

Maj Gen Muhanga alikuwa kamanda wa wanajeshi wanaopambana na wapiganaji wa Al-shabaab nchini Somalia.

Usalama wa jiji la Kampala sasa unaongozwa na wanajeshi kama ifuatavyo:

Maj Gen. Paul Lokech – naibu wa mkuu wa polisi

Maj Gen. Kayanja Muhanga – Kamanda wa usalama jijini kampala

Maj Gen Sam Kawagga - Kamanda wa divisheni ya Kakiri

Maj Gen Leopold Kyanda – kamanda wa wanajeshi wa nchi kavu

Maj Gen Abel Kandiho – Kamanda wa ujasusi katika jeshi

Brig Gen CS Ddamulira – mkuu wa idhara ya usajusi katika polisi

Katika ujumbe wake wa mwaka mpya, rais Museveni amesema kwamba amewateua maafisa wa jeshi wenye ujuzi wa hali ya juu na ambao wamekuwa wakikabiliana na makundi ya wapiganaji kama Allied democratic forced ADF na Al-shabaab nchini Somalia, kuhakikisha kwamba usalama unaimarika jijini Kampala hasa katika maeneo ambayo “polisi wadhaifu na wafisadi” wameshindwa kufanya kazi.

Museveni amesema kwamba wanajeshi hao wataongoza oparesheni za kukabiliana na makundi ya upinzani yanayowatishia rai ana kusababisha vurugu jijini Kampala na sehemu zinazolizunguka jiji hilo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG