WHO : Watoto Afghanistan wakabiliwa na maradhi na utapiamlo

Your browser doesn’t support HTML5

Watoto wa Afghanistan ambao wanakabiliwa na maradhi hatarishi.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ameonya kuongezeka kwa kesi za ugonjwa wa surua na kuharisha nchini Afghanistan na hatari ya utapiamlo kwa Watoto wadogo na kurejea kwa ugonjwa wa polio.

Tedros Adhanom Ghebreyesus alitoa maoni hayo kwa waandishi wa Habari baada ya kuzitembelea hivi karibuni Afghanistan na Lebanon.

Amesema kwa zaidi ya miaka 20 mafanikio muhimu yamepatikana Afghanistan katika kupunguza vifo vya watoto wachanga wakati wa kujifungua, kutokomeza polio, na mengine.

Mafanikio hayo sasa yapo katika hatari kubwa, huku mfumo wa afya ukiwa karibu kuvunjika, amesema mkuu wa WHO.

"Kuna kesi nyingi za surua na kuharisha. Karibu asilimia 50 ya Watoto wako katika hatari ya utapiamlo. Kuzuka kwa ugonjwa wa kupooza ni hatari kubwa na dozi milioni 2.1 za chanjo ya COVID-19 bado hazijatumika. Kama hatua za haraka hazitachukuliwa," amesema Ghebreyesus.

Mkuu wa WHO aliongoza kusema : "Afghanistan itakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu. Wafanyakazi wa afya wanaondoka jambo linaloumiza kichwa kwa sababu ya madhara yatakayotokea kwa miaka ijayo. Tulitembelea hospitali ambako wauguzi wamebaki, moyo wangu uliumia waliponiambia hawajalipwa kwa miezi mitatu.”