Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerrold Nadler alimwalika Rais Donald Trump na mwanasheria wake kuhudhuria kikao hicho cha kwanza cha kamati hiyo inayosikiliza shauri hilo la uchunguzi wa kumfungulia kesi ya kumuondoa rais madarakani ikiingia katika awamu nyingine.
Wakati hakuna aliyekuwa na matarajio ya kuhudhuria kwake, rais amepanga kuhudhuria mkutano wa NATO unaofanyika karibu na London wiki hii, mshauri wa White House Pat Cipollone pia amekataa mwaliko wa Jumatano.
Cipollone alisema atajibu mwishoni mwa wiki iwapo White House itashiriki kwenye shauri hilo katika siku zijazo.
Nadler alimhakikishia Trump na wakili wake katika barua ya mwaliko aliyoituma wiki iliyopita kwamba “anayo nia ya dhati kuhakikisha mchakato huu wa mahojiano ni wa uadilifu na wenye kuelimisha.
Kikao hicho cha Kamati ya Sheria siku ya Jumatano kitalenga kwenye kanuni za katiba zinazoelezea mashtaka ya kuondolewa madarakani rais. Mashahidi ambao bado hawajatajwa majina watakuwa ni wataalamu wa sheria.