Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuomba misaada iimarishwe kwa Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly, ataomba  misaada iimarishwe kwa Ukraine wakati wa zaira yake  Marekani na Canadaambayo inaanza  Jumanne, kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja wa uvamizi wa Russia.

Uingereza imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Kyiv tangu uvamizi wa Russia Februari mwaka jana na mwishoni mwa wiki, iliahidi kuipelekea Ukraine msaada wa vifaru 14 aina ya Challenger 2 na silaha nyingine nzito.

Ujerumani iko katika shinikizo la kutuma Ukraine vifaru aina ya Leopard 2, lakini serikali inasema vifaru hivyo vipelekwe Ukraine pale tu kama yakakuwepo makubaliano baina ya washirika wakuu wa Kyiv hususani Marekani.

Cleverly atamueleza waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzao wa Canada Melanie Joly kuwa huu ni muda muafaka wa “kusonga mbele na kwa haraka zaidi” kuipa misaada ya kijeshi Ukraine.

“ Leo tunasimama pamoja dhidi ya vita haramu vya Putin, na tutaendelea kutumia uhusiano wetu wa kipekee wa ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa hatimaye wananchi wa Ukraine wanashinda” Cleverly ametoa kauli hiyo kabla ya kuanza ziara yake.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza pia imesema, wakati wa ziara hiyo Cleverly atazungumzia suala la Iran, baada ya Uingereza kumrudisha nyumbani balozi wake kwa muda kufuatia hukumu ya kifo ya Alireza Akbari raia wa UIngereza na Iran iliyotolewa Jumapili.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.