Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema sekta ya viwanda vya ulinzi ya Russia huenda ikaamua kutumia mpango wa ajira kwa wale waliokutwa na hatia ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji ya wakati wa vita, katika taarifa ya kijasusi ya Ijumaa kuhusu uvamizi wa Russia nchini Ukraine.
"Mwezi Novemba 2022," ripoti iliyochapishwa kwenye Twitter ilisema, "Uralvagonzavod (UVZ), kiwanda kikubwa kinachotengeneza vifaru cha Russia, iliviambia vyombo vya habari vya ndani kwamba kitaajiri wafungwa 250 baada ya kukutana na Federal Penal Service (FSIN)."
Russia ina historia ndefu ya kuajiri wafungwa na mwaka 2017 "ajira za kulazimishwa kama adhabu maalum kwa uhalifu zilirejeshwa tena," wizara hiyo ilisema.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema, "Idadi ya wafungwa inatoa rasilimali ya kipekee ya binadamu kwa viongozi wa Russia kutumia kuunga mkono "operesheni maalum za kijeshi" wakati watu walio tayari kujitolea bado wapo pungufu."