Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan kutumikia kifungo cha miaka 10 kwa kuanika siri za serikali zinazo husiana na Marekani

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan

Mahakama maalum nchini Pakistan imemhukumu Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan kutumikia kifungo cha miaka 10  jela, Jumanne kwa mashtaka yanayohusiana na kipindi alichokuwa madarakani, akianika siri za serikali kwa umma zinazohusiana na Marekani.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wakati wa utawala wa Khan, Shah Mehmood Qureshi, pia alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka kumi kutokana na kesi inayohusiana na nyaraka za siri maarufu ndani ya serikali kama cipher.

Shah Mehmood Qureshi

Khan alidai nyaraka za kidiplomasia za siri zilikuwa zimesajili jukumu la Marekani katika kuipindua serikali yake ikisaidiwa na jeshi ili kumuadhibu kwa kuisukuma Pakistan kuwa na sera ya kigeni iliyokuwa huru kutokana na ushawishi wa Marekani. Washington na jeshi la Pakistan wamekanusha tuhuma hizo.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan mwenye umri wa miaka 71, ambaye alipinduliwa mwezi Aprili 2022 na muungano wa upinzani, ameipinga kesi hiyo ya cipher akisema ina ushawishi wa kisiasa na imetengenezwa na jeshi lenye nguvu la nchi hiyo.

Chama cha Tahreek-e-Insaf

Chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf, au PTI kimekosoa uamuzi wa mahakama kuwa “ni kebehi kamili na kutoheshimu sheria” katika kesi ambayo “vyombo vya habari vimezuiliwa kuripoti au umma kushuhudia.” Chama hicho kilisema timu yake ya wanasheria “itapinga maamuzi ya mahakama ya juu” na “ina matumaini itaweza kufanya hukumu hii kusitishwa.”

Mahakama hii yenye jaji mmoja aliyeendesha kesi ndani ya gereza lenye ulinzi mkali karibu na Islamabad, bila ya kuruhusu wawakilishi wa vyombo vya habari wa nje au vyombo vikuu vya habari vya Pakistani kuhudhuria.

Hukumu iliyofikiwa Jumanne ya kumkuta na makosa chini ya Sheria ya Official Secrets imekuja kabla ya uchaguzi wa bunge kufanyika Pakistan, ambao umepangwa Februari 8.

Ripoti ya mwandishi wa VOA Ayaz Gul.