Jeshi la Mali limethibitisha kupitia mitandao ya kijamii kwamba mji wa Lere, uliko katika mkoa wa Timbuktu kaskazini mwa Mali, ulishambuliwa siku ya Jumapili.
Afisa wa jeshi la Mali ameliambia shirika la habari la AFP kuwa jeshi "liko katika harakati za kukabiliana na hali hiyo."
"Baada ya mapigano, watu wenye silaha walizikamata kambi. Tunasubiri nguvu kutoka jeshini, lakini kwa wakati huu ni watu wenye silaha wanazishikilia hizo kambi," aliongeza.
Afisa utawala wa mkoa, pia alisema watu wenye silaha wamezishambulia kambi hizo mbili na kuendelea kuzishikilia.
Alisema kumekuwa na vifo lakini hakuweza kutoa idadi.
Almou Ag Mohamed, msemaji wa Coordination of Azawad Movements, muungano wa makundi yenye silaha yanayotaka kujitenga yanayoongozwa na kabila la Tuareg, amedai kuhusika na shambulio hilo.
Makundi yanayotaka kujitenga walianzisha uasi mwaka 2012, kabla ya mkataba wa amani na serikali kutiwa saini mwaka 2015. Lakini kwa ujumla, makubaliano hayo sasa yanachukuliwa kuwa ya kufa.
Mwezi huu makundi hayo yameshuhudia kuanzisha tena uhasama.
Siku ya Jumanne, makundi hayo yalianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya jeshi yaliyoko katika mji wa Bourem, ambayo wanajeshi walisema waliweza kuyaondoa.