Watu wasiopungua 25 hawajulikani waliko baada ya maporomoko ya ardhi kutokea Myanmar

Maporomoko ya ardhi Myanmar.

Watu wasiopungua 25 hawajulikani waliko baada ya maporomoko ya ardhi kutokea katika machimbo yasiyo rasmi ya Jade katika eneo la ndani la Myanmar, wafanyakazi wa uokoaji walisema Jumatatu.

Tukio la Jumapili nje ya mji mdogo wa Hpakant ulioko kaskazini mwa Kachin – karibu na ambako mamia ya wachimba madini walifukiwa na maporomoko ya ardhi ya mwaka 2020 – limekuja siku kadhaa baada sehemu kubwa ya nchi kupata mvua kubwa na mafuriko.

Sekta ya uchimbaji madini iliyokuwa na biashara kubwa sehemu kubwa haijarasmishwa, huku wafanyakazi wahamiaji wakikabiliana na hali ya hatari na matukio ya vifo.

“Takriban watu 25 hawajulikani waliko. Hatujapata orodha kamili na ni vigumu kufika katika eneo hilo,” mmoja wa wafanyakazi wa uokoaji, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia shirika la habari la AFP kutoka katika eneo la tukio la ajali hiyo.

Alieleza namna rundo la kifusi lenye ukubwa wa mita 150-180 lililoachwa na wachimbaji madini lilivyosambaratishwa na mvua kubwa na kuporomoka.

Harakati za msako na uokoaji zinaendelea, alisema, lakini baadhi ya wafanyakazi walikuwa tayari wamerejea katika eneo la tukio kwa matumaini ya kutafuta waliokuwa katika machimbo ya jade.

“Hatujapata miili yoyote hadi sasa,” alisema.

Mfanyakazi mwingine wa uokoaji aliithibitishia AFP kuwa juhudi za kuwatafuta watu zinaendelea licha ya hofu ya kuwepo maporomoko madogo madogo.

“Siyo salama kwa wafanyakazi wa uokoaji kuendelea kutafuta watu katika eneo hilo la mchimbo,” alisema mtu mmoja, ambaye alikuwa na kikundi cha dharura cha uokoaji cha Myanmar na kuaomba asitajwe jina lake.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.