Baadhi ya wananchi waliiambia Sauti ya Amerika kuwa mbali na uhaba huo bei ya sukari imepanda kwa kiasi kikubwa, kutoka shillingi 2800 mwezi Disemba hadi kufikia shillingi 4000 mwezi Februari huku kwa baadhi ya maeneo ikipatikana kwa shillingi 6000.
Bujiku Budo mkazi wa Mwanza amesema kwa kipindi kirefu bei ya sukari imekuwa haina utulivu, imekuwa ikipanda na kushuka mara kwa mara suala linaloendelea kuwaathiri kiuchumi na kijamii.
“Wakati wa nyuma sukari ilikuwa inauzwa shillingi 2600 baadaye ikaanza kupanda mia mia mpaka ikafikia shillingi 3000 ilipofika 3000 ikaanza tena kupanda kwa mia mbili mia mbili mpaka ikafika shillingi 3800. Rais alipokuja huku mwanza ikashuka mpaka 3500 alipotoka tu muda mfupi ikapanda hadi kufikia 4200 kwa hali inayotuathiri kiuchumi.” alisema Budo
Naye Butige Khamisi mkazi wa Ilemela Mwanza amesema licha ya serikali kusema inaagiza sukari kutoka nje ya nchi lakini bado wananchi wa kawaida hawajaona nafuu inayoletwa na sukari hiyo inayoagizwa na hali inazidi kuwa mbaya kila siku na hivyo ameitaka serikali kukaa na wafanyabiashara ili kutatua changamoto hiyo.
“Serikali imesema imefungua milango kwa baadhi ya wafanyabiashara walioruhusiwa kuweza kuingiza sukari lakini hata hizo jitihada zinazofanyika na tumesikia sukari tani kwa tani imeingia nchini lakini bado hatujaona ile nafuu sukari tunaambiwa inaletwa” alisema Khamisi.
Aliongeza kwa kusisitiza kwamba “lakini hatujaona nafuu nadhani kuna sehemu serikali na wafanyabiashara bado hawajaweza kukaa vizuri na kuhakikisha kwamba sukari inapatikana nchini.”
Ikielezea uhaba huo wa sukari uliosababisha bei kupanda kwa kiasi kikubwa, Bodi ya Sukari Tanzania imedai kuwa hali hiyo imesababishwa kwa sehemu na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyopelekea baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji kutokan na mvua.
Mkurugenzi wa bodi hiyo Keneth Bengezi ameiambia Sauti ya Amerika kuwa serikali imeendelea kuagiza sukari kutoka nje na imetoa kibali kwa tani 100,000 ya sukari kuingia nchini, wakati tani 6,070 zimeshaingia na kiwango kikubwa cha sukari kinatarajiwa kuingia nchini ili kupunguza uhaba huo.
“Sukari imekwisha kuanza kuingia tayari tuna tani karibu kama elfu sita na sabini ambayo ipo tayari nchini na nyingine inaendelea kuingia lakini mwezi huu kati kati tutakuwa tumeingiza zaidi ya tani elfu thelathini kwahiyo kama unavyojua uagizaji ni mchakato, tunavyosema imeanza kuingia ndivyo tunakwenda kuendelea kupokea na tutapata kiasi cha kutosha ambacho kitaondoa tatizo hili.” amesema Bengezi
Hata hivyo, wafanyabiashara wadogo nchini wanapinga bei elekezi ya sukari iliyowekwa na serikali kutokana na bei hiyo kutolingana na uhalisia wa soko na hivyo kuendelea kuleta hasara kwenye biashara zao.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani. Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.