Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 13:55

Wamiliki wa vyombo vya habari Tanzania walalamikia kutokua na uhuru


Mwanamke mkimbizi akiwa amebeba redio akiwa kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika Picha na REUTERS/Thomas Mukoya
Mwanamke mkimbizi akiwa amebeba redio akiwa kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika Picha na REUTERS/Thomas Mukoya

Kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari kutoa baadhi ya habari pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya kodi na tozo ni miongoni mwa changamoto zinazosababisha ugumu katika uendeshaji wa vyombo vya habari nchini Tanzania .

Katika kuadhimisha siku ya radio duniani, wamiliki wa vyombo vya habari na wadau wa habari Tanzania wamesema kuwa kukosekana kwa uhuru katika kuchapisha habari za siasa pamoja na tiba mbadala kuna sababisha kupoteza mapato na kuwepo kwa ubaguzi wa habari.

Angela Aweda, Mkurugenzi wa Redio Maisha fm iliyopo Dodoma amesema kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari kumewasababisha kuogopa kukaribisha viongozi wa vyama vya upinzani kwa kuhofia kufungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Changamoto moja wapo ni ufinyo wa uhuru kwenye vyombo vya habari kwenye upande wa siasa unashindwa kukaribisha hata watu wa siasa kuzungumza kwenye chombo cha habari kwasababu wakiongea kitu chochote kwa mfano upande mwingine wa upinzani yaani unaogopa, unahofu atazungumzia nini akikosea tu kidogo unajua kesho nitakuja kufungiwa kwa hiyo tunakuwa hatuna uhuru," alisema Aweda .

Changamoto nyingine ambayo vyombo vya habari vimekuwa vikikutana nayo ni pamoja na kuwepo kwa mrundikano wa kodi na tozo serikalini ikiwemo kodi za TRA tozo ya mfuko wa mawasiliano (USCAF) tozo ya usimamizi wa ulinzi na usalama kazini (OSHA) pamoja na ushuru wa huduma yaani service levy.

Amosi Ngosha Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari vya Utangazaji Tanzania (NIBA) amesema vyombo vya habari vingi vimeshindwa kuendelea kutokana na kuwepo wa idadi kubwa ya tozo ambazo zinapaswa kulipwa kutokana na mapato ghafi ya wamiliki wa redio hizo.

“Kingine kinachotuangusha kuna tozo za serikali zaidi ya ishirini na saba 27 zipo kwenye mfumo wetu wa redio kwaajili ya kuilipa serikali hizo tozo kwa asilimia mbalimbali” alisema Ngosha.

“Tena unapewa hizo tozo kwenye mapato ghafi ndio unapewa hiyo tozo ili utoe kila unapotakiwa kwa mwaka kwahiyo vyombo vya habari vimejikuta kwenye changamoto kubwa kwenye uendeshaji wake,” aliongeza.

Hata hivyo Dkt Wilfred Rutahoile moja wa mdau wa masuala ya redio na utangazaji amesema kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari kumepelekea wasikilizaji kuhama na kuanza kusikiliza vyombo vya nje za nchi zaidi kuliko vyombo vya ndani kutokana na vyombo hivyo kushindwa kuchapisha maudhui yanayogusa maisha yao moja kwa moja.

“Unapokuja kunyima uhuru vyombo vya ndani utakuta watu wanapendelea kusikiliza vyombo vya majirani kuliko kusikiliza vyombo vya ndani kwasababu wanasema vyombo vya ndani vimebanwa vinatoa vitu ambavyo havigusi maisha yao moja kwa moja kwahiyo wanachagua zaidi kusikiliza majirani wanasemaje kwasababu watu wapo huru kusema wanachokitaka.” alisema Rutahoile

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Redio: Karne ya kutoa habari, kuburudisha na kuelimisha." huku Ngosha akimalizia kwa kuitaka serikali ya Tanzania kupitia upya sera na sheria zilizopitwa na wakati zinazonyima uhuru kwa vyombo vya habari ili kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa huru.

Amri Ramadhani sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG