Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:02

Wachambuzi wahoji kauli ya Rais Samia kulitaka jeshi kujitayarisha kwa ajili ya uchaguzi


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri jeshi mkuu Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Jenerali Jacob John Mkunda. Picha na Ikulu Mawasiliano
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri jeshi mkuu Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Jenerali Jacob John Mkunda. Picha na Ikulu Mawasiliano

Wachambuzi Tanzania wamedai kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulitaka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujiandaa kukabiliana na chochote wakati wa uchaguzi kuwa ni tishio kwa demokrasia.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika wametaka ufafanuzi utolewe ili kuepusha mikanganyiko katika nchi hiyo ambayo inatarajia kuwa na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024 na 2025.

Aidha wamesema kuwa suala la uchaguzi ni suala la kiraia na jeshi la ulinzi wa wananchi wa Tanzania halipaswi kuingilia kwenye masuala ya uchaguzi ili kuepusha kuleta wasiwasi miongoni mwa wananchi na wanasiasa.

Mhadhiri wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Richard Mbunda amesema kulitaka jeshi la wananchi kuingilia masuala ya uchaguzi inaonesha kuwa pengine uchaguzi unakuwa haufanyiki katika mazingira ya salama.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kwamba vyombo hivi vimekuwa vinatumika kutengeneza matokeo kwahiyo unapotoa kauli kama hizo unakuwa unajaribu kuthibitisha zile hisia za wananchi kwamba yawezekana uchaguzi haufanyiki katika mazingira ya uwanja sawa yawezekana kwamba kuna vyombo vinavyotumika ambavyo vilitakiwa visiingilie masuala ya uchaguzi.” Amesema Mbunda.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa Jeshi. Picha na Ikulu Mawasiliano
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa Jeshi. Picha na Ikulu Mawasiliano

Wachambuzi wanasema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina majukumu ya msingi ikiwemo kulinda katiba na uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi wa mipaka pamoja na kushirikiana na mamlaka za kiraia kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa lakini kushiriki katika uchaguzi ikiwa sio miongoni mwa majukumu yao.

Sabatho Nyamsenda ni mhadhiri msaidizi wa idara ya sayansi ya siasa na utawala wa umma kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema serikali inapaswa kuhakikisha shughuli za kisiasa haziingiliani na masuala ya jeshi na iwapo chama cha siasa kitakiuka sheria ya vyama vya siasa basi kinapaswa kufutwa kwa mujibu wa sheria na sio kutegemea dola.

“Kuchukua hatua za kisheria na kikatiba za kuhakikisha kwamba shuguli za kisiasa zinabaki kuwa za kisiasa na kama vyama vya siasa havifanyi shuguli zao kwa mujibu wa sheria,” alisema Nyamsenda na kuongeza kuwa

“sheria iko wazi vinatakiwa kuondolewa lakini kama vinafanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria basi ni vyema vikaachwa kufanya shughuli zao na ukatengenezwa uwanja ambao ni tambalale kati ya vyama vya siasa na chama tawala ili chama tawala kisitegemee dola kubaki madarakani.”

Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi wakisheherekea ushindi wakati wa uchaguzi wa Rais Oktoba 30, 2020.
Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi wakisheherekea ushindi wakati wa uchaguzi wa Rais Oktoba 30, 2020.

Hata hivyo Mbwana Aliamutu Mchambuzi wa siasa kutoka Morogoro amesema kauli ya Rais inaweza kuleta mitazamo tofauti kwa vyama vya upinzani na kuonyesha kurudisha nyuma jitihada za demokrasia ya nchi na kuonyesha vitisho kwa vyama hivyo kuelekea chaguzi za serikali kuu na serikali za mitaa.

“Vyama vya upinzani vinaweza vikaitazama kauli hii kwamba ni kauli inayorudisha nyuma jitihada kubwa za demokrasia kwa nchi ya Tanzania na wanaweza wakaitazama pia kama kauli ya vitisho kuonyesha dira ya kuelekea kwenye uchaguzi kutakuwa na utumiaji wa dola na nguvu kwa maana ya vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kulinda chama kilichopo madarakani.”

Hata hivto Dkt Mbunda ameitaka serikali kutoa ufafanuzi juu ya kauli hiyo ili kuepusha tafsiri tofauti zinazotolewa na wadau mbalimbali wa demokrasia nchini Tanzania.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG