Wasiwasi wa kuvunjika kwa sitisho la mapigano waongezeka Sudan

Mwanamume akiendesha gari lake la kukokotwa na punda wakati mapigano yalipopungua. Picha na AFP.

Mapigano ya hapa na pale kati ya jeshi la Sudan na kikosi chenye nguvu cha wanamgambo wa RSF yaliendelea mpaka siku ya Alhamisi, na kuathiri hali ya utulivu katika mji mkuu wa Khartoum na kuongeza wasiwasi wa kusambaratika kwa makubaliano ya kimataifa ya wiki moja.

Sitisho la mapigano ambalo lilikuwa chini ya usimamizi wa Saudi Arabia na Marekani pamoja na pande zinazozozana, lilifikiwa baada ya wiki tano za vita huko Khartoum na kusababisha ghasia katika maeneo mengine ya Sudan, ikiwemo mkoa wa magharibi wa Darfur.

Mapigano hayo kati ya jeshi la Sudan dhidi ya wanajeshi wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) yamezidisha mzozo wa kibinadamu, na kuwafanya watu zaidi ya milioni 1.3 kuyakimbia makazi yao na kutishia kuiyumbisha kanda hiyo.

Jeshi, likiongozwa na afisa mzoefu Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, linategemea nguvu za anga wakati vikosi vya RSF, vinayoongozwa na kiongozi wa zamani wa wanamgambo Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu kwa jina la Hemedti, wameenea na kujificha katika mitaa ya Khartoum.

Haijabainika ni upande upi umepata mafanikio katika mzozo ambao unatishia kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu na kuziyumbisha nchi zilizoko katika kanda hiyo.

Mapigano kati ya makundi hasimu ya kijeshi yalizuka siku ya Jumatano katika jiji la Khartoum na miji mingine, wakazi walisema.

Kwa muda wa siku chache zilizopita, mji wa Zalingei, ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Darfur ya Kati, umekuwa ukizingirwa na wanamgambo wenye silaha, wakati mratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kwa Darfur, Toby Harward alitoa wito kwa mamlaka kuudhibiti tena wa mji huo.

Hakuna mawasiliano ya simu, huku magenge ya wahuni yakiwa kwenye pikipiki yakizunguka jijini yakishambulia hospitali, ofisi za serikali na za misaada, benki na nyumba.

Sitisho la mapigano lilikubaliwa siku ya Jumamosi kufuatia mazungumzo yaliyofanyika mjini Jeddah yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani. Matangazo ya awali ya sitisho la mapigano hayo hayakuzaa matunda.

Katika taarifa iliyotolewa mwishon Jumatano jioni , jeshi la Sudan na vikosi vya RSF vinashutumiana kila mmoja akiuka makubaliano.