Ndege hiyo ya kubeba mizigo aina Antonov 72 ilipotea angani baada ya kuruka kutoka mjini Goma kuelekea katika mji mkuu Kinshasa. Mamlaka ya usafiri wa anga imethibitisha kwamba ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na kituo cha usafiri wa anga kuanzia saa tisa mchana majira ya DRC. Mamlaka hiyo inasema watu 8 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wamefariki.
Radio OKAPI ya Umoja wa Mataifa ikinukuu vyanzo vya ikulu ya DRC imesema watu 27, wakiwemo walinzi wa Rais Tshisekedi, dereva wake na wasaidizi wake ndio waliokuwa ndani ya ndege hiyo, na wote wanahofiwa wamefariki.
Taarifa zimeendelea kusema kwamba mabaki ya ndege hiyo iliyoanguka yaliokotwa katika jimbo la Maniema.
Hayo yakiarifiwa, wafuasi wa chama cha UDPS cha Rais Felix Thisekedi wameandamana Ijumaa asubuhi katika barabara za mji mkuu Kinshasa, ili kuonyesha hasira zao kutokana na kupotea kwa ndege hiyo. Waandamanaji hao ambao wamechoma matairi na kuweka vizuizi barabarani, wanaomba uchunguzi ufanyike ili kujuwa kilichosababisha ajali ya ndege hiyo.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.