Kwa Mujibu wa taarifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mkutano wa 18 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama, ulipokea na kutafakari taarifa ya baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo kuhusu ujumbe wa uhakiki wa kukubaliwa kwa DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuliagiza baraza kuanza haraka na kumaliza mazungumzo na DRC kwa ajili ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Yoweri Museveni, Rais wa Uganda ameeleza: “nimefurahi leo tumethibitisha mchakato wa kuwaandikisha Congo kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama nilivyoeleza katika mkutano wetu wa ndani, Congo ni sehemu ya Afrika Mashariki kihistoria. Eneo la Mashariki wanazungumza Kiswahili, makabila yao ni kama ya huku katika nchi zetu, ukoloni ndio uliiweka Congo eneo tofauti na Afrika Mashariki.
Samia Suluhu, Rais wa Tanzania: “Sote tunafahamu umuhimu wa Congo kujiunga na jumuiya yetu, nchi zetu zimekua na ushirikiano na urafiki wa karibu na Congo kwa muda mrefu iwe kibiashara ama ujirani. Na hii itaongeza ustawi wa watu wetu na ukanda mzima kwa ujumla, zaidi ya hayo DCR inajiunga na ndugu zake’
Paul Kagame, Rais wa Uganda ameeleza: “Rwanda inakaribisha maendeleo yaliyofikiwa katika mchakato wa kuipa uanachama Congo. Tunatarajia hitimisho la haraka kwa taratibu zilizobaki.”
Awali Katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Peter Mathuki aliueleza mkutano huo kuwa tayari wamekwisha kamilisha hatua 7 kati ya Kumi kuelekea kukamilisha mchakato wa kuipa uanachama DR. Congo.
Peter Mathuki, Katibu Mkuu EAC : "Kufuatia maelekezo yenu na ushirikiano mliotupatia tumekamilisha hatua zinazotakiwa saba kati ya 10, nashurukuru kwa ushirikiano mliotupatia."
Maamuzi haya yanaelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa hatua muhimu kwa Jumuiya ya Afrika mashariki kwani itaongeza tija zaidi katika baadhi ya sekta ikiwemo ya Biashara kwa kupanua soko.
Mkutano huo pia ulilielekeza Baraza hilo kuharakisha kuanza na kuhitimisha mazungumzo na DRC kwa ajili ya kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuripoti katika mkutano ujao,” ilieleza taarifa iliyotolewa baada ya mkutano.
Wakuu wa nchi pia walielekeza Sekretarieti ya EAC kuleta ripoti juu ya mapendekezo ya kurekebisha vifungu vya Mkataba wa EAC unashughulikia koram ya mikutano.
Pia walimkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amemrithi hayati John Magufuli, ambapo alitoa hotuba yake ya kwanza.
Vyanzo vya habari hii ni VOA na Gazeti la The East African la Kenya