Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 10:56

Mahakama ya EAC yatupilia mbali kesi ya kumzuia Museveni kugombea urais


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika mashariki imetupilia mbali kesi dhidi ya mabadiliko ya katiba nchini Uganda yaliyotoa nafasi kwa rais Yoweri Museveni kugombea muhula mwingine madarakani.

Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Monica Mugenyi Jumatano, mahakama hiyo imeamua kwamba “hatua ya kuondoa ukomo wa umri kwa wagombea wa urais nchini Uganda haikukiuka katiba ya Uganda.”

Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha, Tanzania, imemwondolea pia makosa aliyekuwa jaji mkuu wa Uganda Bart Katureebe katika kesi hiyo iliyowasilishwa na wakili wa Uganda Male Mabirizi.

Wakili huyo alikuwa amemshutumu Katureebe kwa kufanya kazi yake bila kuzingatia maadili na kuwa na upendeleo.

Kuhusu kesi iliyowasilishwa

Katika kesi yake, wakili Mabirizi alidai kwamba mchakato mzima wa kubadilisha kifungu 102(b) cha katiba ya Uganda, kilichokuwa kimeweka ukomo wa miaka 75 kwa wagombea wa urais nchini Uganda, haukufuata sheria.

Kesi hiyo ilifikishwa katika mahakama ya jumuiya ya Afrika mashariki mwezi May, 2019, ikitaka hatua ya kufanyia marekebisho katiba ya Uganda kufutiliwa mbali.

Majaji 4 kati ya 3 wa mahakama ya juu kabisa nchini Uganda walitupilia mbali rufaa ya wakili Mabirizi kwa msingi kwamba licha ya kuwepo dosari katika mchakato wa kufanyia marekebisho katiba hiyo, dosari hizo hazikuathiri mchakato mzima.

Aliyekuwa jaji mkuu Bert Katurebe, majaji Stella Arach Amoko, Rubby Opio Aweri na Jotham Tumwesigye waliidhinisha mabadiliko hayo ya katiba huku majaji Eldad Mwangusya, Lilian Tibatemwa na Paul Mugamba wakikubaliana na wakili Mabirizi, ambaye baada ya kutoridhika na maamuzi hayo, alikata rufaa katika mahakama ya jumuiya ya Afrika mashariki.

Utetezi wa serikali ya Uganda katika mahamakama ya EAC

Katika kuwasilisha utetezi wa serikali katika mahakama ya jumuiya ya Afrika Mashariki, mwanasheria mkuu wa Uganda Gerald Byaruhanga alisisitiza kwamba wakili Mabirizi alikuwa anatumia njia za ujanja kumaliza muda wa mahakama, kwani kesi hiyo ilikuwa tayari imeamuliwa na mahakama ya juu kabisa Uganda na kwamba hakukuwa na haja tena ya kufunguliwa upya ndani wala nje ya Uganda.

Byaruhanga pia alieleza mahakama kwamba katika kufanyia marekebisho ibara ya ukomo wa umri kwa wagombea wa urais, bunge la Uganda lilizingatia mkataba wa jumuiya ya Afrika mashariki na kanuni zote za kidemokrasia.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG