Balozi za Marekani
Balozi za Marekani katika nchi kadhaa zilikabiliwa na waandamanaji, walioghadhibishwa na kifo cha George Floyd kilichotokea Mei 25. Floyd alifariki baada ya polisi mzungu kuweka goti lake kwenye shingo lake kwa takriban dakika 9. Tukio hilo lilirikodiwa katika video, na Floyd alisikika akimlilia polisi mara kadhaa, "Siwezi kupumua."
Berlin Ujerumani
Huko Berlin Jumamosi, maelfu ya Wajerumani walikusanyika nje ya Ubalozi wa Marekani, wakiimba “Uhai wa Watu Weusi ni Muhimu,” kwa mujibu wa chanzo cha habari Forbes.
Toronto Canada
Maadamano juu ya ubaguzi kwa jumla yaliwaleta pamoja maelfu ya watu Jumamosi huko Toronto, Forbes imeripoti.
Ijumaa, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, akizungumzia kifo cha Floyd, amesema katika Makala ya gazeti la The Washington Post, “Ubaguzi uko. Uko nchini Marekani, lakini pia uko Canada. … Tunafahamu watu wanakabiliwa na mfumo wa ubaguzi, kuegemea upande mmoja na ubaguzi dhidi ya watu weusi bila ya kujitambua kila siku.
Mexico City
Huko Mexico City Jumamosi, michoro na maua yalioandaliwa kwa ajili ya kumkumbuka Floyd yalitundikwa katika senyenge karibu na Ubalozi wa Marekani, kwa mujibu wa taarifa zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Umoja wa Mataifa
Siku ya Ijumaa, Kamishna wa Umoja wa Mataifa juu ya Masuala ya Haki za Binadamu Michelle Bachelet pia alilaani mazingira yaliopeleka kifo cha Floyd, ambapo alisema ni tukio la karibuni “katika mlolongo wa mauaji ya Wamarekani weusi wasiokuwa na silaha yaliofanywa na maafisa wa polisi wa Marekani na watu wengine katika jamii.
“Nimesikitishwa kwamba hivi sasa naongeza jina la George Floyd ikiwa katika orodha ya wengine waliouawa akiwemo Breonna Taylor, Eric Garner, Michael Brown na Wamarekani weusi wengine waliouawa wakiwa hawana silaha kwa miaka mingi katika mikono ya polisi – na wengine kama vile Ahmaud Arbery na Trayvon Martin waliouawa na watu wengine katika jamii,” ameeleza.
Dalai Lama
Kiongozi wa kiroho wa Tibet, Dalai Lama, amesema ameona picha za video ya Floyd akiwa amelala chini huku polisi akimwekea goti lake juu ya shingo yake.
“Kwa sababu ya ubaguzi huu kutokana na rangi ya mtu, mambo kama haya yanafanyika,” amesema wakati wa maombi kupitia tovuti Ijumaa.
“Tunashuhudia katika vituo vya habari, vyombo vya habari, juu ya ubaguzi kwa sababu ya rangi ya mtu au dini siku hizi, halafu kuna mauaji kutokana na ubaguzi, na kuna wengine wanajigamba kwa vitendo hivyo kwa kuweza kumuua mtu.”
Umoja wa Afrika
Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Ijumaa ilitoa kauli kali ambayo ni nadra kutolewa kwa umma juu ya matukio ya ndani ya nchi ya Marekani.
Katika tamko hilo, mkuu wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat, “alilaani vikali” mwenendo wa polisi katika kesi ya Floyd na kutoa “rambirambi za dhati kwa familia na wapendwa wa Floyd.”