Mkutano huo wa 38 wa mataifa 7 ya IGAD uliitishwa na Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok ambaye ni mwnyekiti wa jumuia hiyo kujadili miongoni mwa masuala mengine, ugomvi wa ndani nchini Ethiopia, mapigano ya mpakani kati ya Ethiopia na sudan pamoja na mvutano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia.
Katika kikao cha ufunguzi mwenyeji wa mkutano Rais Ismail Guelleh alipongeza juhudi zilizopatikana katika kudumisha amani na utulivu katika kanda hiyo licha ya kuwepo kwa janga la Covid-19 na majanga mengine ya mafuriko na uvamizi wa nzige.
Mkutano huo unahudhuriwa pia na mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, aliyesema kwenye kikao hicho cha ufunguzi kwamba mvutano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia unazusha wasi wasi kwenye Umoja wa Afrika.
Mahamat ametoa wito wa kuwepo na majadiliano kupunguza mvutano uliyopo akisema nchi hizo mbili zina historia ndefu ya ushirikiano mzuri na zinalazimika kutanzua matatizo yao kwa majadiliano.
Kuhusiana na Ethiopia mwenyekiti wa Kamisheni ya AU amewahimiza wanachama wa IGAD kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na janga la kibinadamu linalotokana na vita katika jimbo la Tigray.
Hamdok amesema ameitisha mkutano huo hasa baada ya kuombwa kuwa mpatanishi kwenye ugomvi kati ya Kenya na Somalia, lakini pia ugomvi wa mpakani unaoweza kuzuka kati ya Sudan na Ethiopia, hali huko Sudan Kusini kuna ugomvi kati ya Ethiopia na Somalia.
Mkutano huo unaohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Makamu Rais wa Sudan Kusini Rebecca Garang na Uganda ina wakilishwa na balozi wake nchini Djibouti Rebecca Otengo.