Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 11:30

Somalia yaamuru wanadiplomasia wa Kenya kuondoka Mogadishu ndani ya siku 7


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Abdullahi Farmaajo
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Abdullahi Farmaajo

Serikali ya Somalia imetangaza kusitisha uhusiano wake na Kenya ikidai kwamba serikali ya Kenya inaingilia kati maswala yake ya ndani.

Nchi hiyo jirani wa Kenya, imetangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walio Nairobi kurudi Mogadishu ndani ya siku saba kuanzia leo jumanne Desemba 15 2020.

Waziri wa habari wa Somalia Osman Abukar Dubbe, amesema katika hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja na televisheni ya serikali ya Somalia Jumatatu jioni kwamba hatua hiyo imechukuliwa kujibu uchokozi wa kisiasa wa kila mara unaofanywa na serikali ya Kenya kinyume na uhuru wa Somalia.

Serikali ya Kenya haijajibu madai wala hatua hiyo ya Somalia.

Somalia ilimuondoa balozi wake nchini Kenya Novemba 29 na kuamuru balozi wa Kenya kuondoka Mogadishu.

Wakati huo, Somalia iliishutumu Kenya kwa kuingilia kati maswala yake ya ndani na siasa za nchi hiyo.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, Somalia ilidai kwamba Kenya ilikuwa “inamshinkiza kisiasa” kiongozi wa eneo la Somali Ahmed Mohamed Islam maarufu kama Ahmed Madobe wa Jubaland, ili kutimiza malengo yake ya kisiasa na kichumi ndani ya Somalia.

Somalia inadai kwamba kutokana na ushawishi wa Kenya, Ahmed Madobe alilegeza msimamo wake kuhusu mkataba wa Septemba 17, kati ya serikali kuu na viongozi wa maeneo.

Mkataba huo ulikuwa wa kutoa fursa ya kufanyika uchaguzi usio wa moja kwa moja nchini Somalia lakini kiongozi wa Jubaland sasa anataka serikali ya Somali kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Gedo ili utawala wake uandae uchaguzi. Hatua hiyo inapingwa na serikali kuu.

Kenya na Jubaland zimekanusha madai hayo.

Serikali ya Kenya imeeleza masikitiko kwamba “hatua ya Somalia ilikuwa ya kusikitisha” na kwamba madai hayo “yalikuwa yasiyo na msingi wowote.”

Mgogoro waongezeka zaidi

Mgogoro kati ya Somalia na Kenya umeongezeka zaidi kufuatia ziara ya rais wa Somaliland, ambayo ilijitangazia uhuru kutoka kwa Somalia Muse Bihi Abdi nchini Kenya.

Abdi alikutana na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta jumatatu.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba viongozi hao wawili wamezungumzia maswala “ya muhimu yanayohusu nchi hizo mbili.”

Kenya imesema kwamba haina upendeleo wowote wa kidiplomasia nchini Somaliland lakini imetaja Somaliland kuwa mshirika muhimu sana katika pembe ya Afrika katika kupambana na ugaidi hasa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab.

Kenya imesema kwamba inazingatia sana namna ya kuimarisha biashara na uekezaji kati yake na Somaliland.

Somaliland alijitangazia kujitawala kutoka kwa Somalia mnamo May 1991 lakini uhuru wake haujatambuliwa kimataifa.

Serikali ya Somalia inasisitiza kwamba Somaliland ni sehemu ya Somalia.

Mnamo July mwaka huu, Somalia ilisitisha uhusiano wake na Guinea, baada ya nchi hiyo ya Afrika magharibi kumkaribisha rais wa Somaliland mjini Conakry.

Licha ya uhusiano wa Kenya na Somalia kuwa mbaya katika siku za hivi karibuni, Kenya ina maelfu ya wanajeshi wake nchini humo, chini ya muungano wa Afrika – AMISOM, wanaopambana na wanamgambo wa Al-shabaab.

Nchi hizo mbili vile vile zina mzozo wa mpaka unaosubiri kutatuliwa na mahakama ya haki ya kimataifa.

Kesi hiyo ya mpaka imepangiwa kusikilizwa mjini Hague, March 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG