Vifo vinavyotokana na kimbunga Ana vimeongezeka kufikia 12 Msumbiji na Malawi

Waathirika wa mafuriko nchini Msumbiji

Idadi ya vifo kutokana na dhoruba ya kimbunga Ana imeongezeka na kufikia 12 nchini Msumbiji na Malawi, maafisa wamesema ingawa maafisa na mashirika ya misaada bado wanafanya tathmini ya athari za kimbunga kilichopiga upande wa Kusini mwa Afrika Jumatatu.

Taasisi ya taifa ya msumbiji ya udhibiti na kuzuiya hatari ya majanga jumanne ilisema watu nane wamekufa, wengine 54 wamejeruhiwa na 895 wamehamishwa katika saa 24.

Zaidi ya watu 20,000 nchini Msumbiji wameathiriwa na kimbunga hicho, kukiwa na nyumba zaidi 3,000 zilizoharibiwa kiasi na zaidi ya 600 zimeharibiwa kabisa Pamoja na vituo vya afya mbalimbali na dazeni za madarasa.

Taasisi hiyo imeongeza kusema ndege zisizokuwa na rubani na boti zimepelekwa kwa ajili ya kusaidia katika juhudi za misaada.

Katika nchi jirani ya Malawi kimbunga kimesababisha kukatika umeme kwa kiasi kikubwa wakati mafuriko yakiharibu mitambo ya umeme.

Mkuu wa wilaya ya Chikwawa amethibitisha vifo vingine vitatu baada ya idara ya maafa Jumanne kuripoti kifo kimoja huko Milanje.

Msumbiji na nchi nyingine za kusini mwa Afrika zimerudia kuathiriwa na dhoruba na vimbunga katika miaka ya karibuni ambavyo vimeharibu miundo mbinu na kukosesha makazi idadi kubwa ya watu.