Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amewafuta kazi mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani, akihoji uwezo wao wa utendaji kazi wakati nchi hiyo ikipambana na uasi wa wanamgambo wa kiislamu kwa miaka minne sasa.
Ofisi ya rais Nyusi Jumatano ilitoa taarifa, ikitangaza kwamba waziri wa ulinzi Jaime Neto ameondolewa kwenye majukumu yake.
Siku moja kabla, taarifa kama hiyo ilitangaza kufukuzwa kazi kwa waziri wa mambo ya ndani Amade Muquidade.
Hakuna maelezo yaliyotolewa juu ya kufutwa kazi kwa mawaziri hao muhimu, ambao waliteuliwa miaka miwili iliyopita.
Jumatano Nyusi alisema “ kiongozi au kamanda katika sekta ya ulinzi na usalama hawezi kumudu kulala kazini, hasa nyakati za vita”, alisema katika hotuba wakati wa sherehe za wanajeshi wa cheo cha sajenti waliohitimu.
Ameongeza kuwa “ vyeo mnavyoshikilia haviwaruhusu kuwa wazembe, majukumu yenu yako wazi, wanajesji lazima watetee taifa”.