Wakati huohuo Kyiv ilifunga upitishwaji wa gesi kupitia eneo linaloshikiliwa na Russia na hivyo kuibua wasiwasi wa kuwepo mzozo wa nishati Ulaya.
Katika kijiji cha Vilhivka mashariki mwa Kharkiv kinachoshikiliwa na vikosi vya Ukraine milio ya risasi, na roketi vilisikika kutokana na mapigano ambayo sasa yamesonga mbele zaidi mashariki ambako Ukraine imekuwa ikijaribu kukamata kingo za mto Donets na kutishia njia za usambazaji wa Russia upande wa mbali.
Kufuatia kusonga mbele kwa siku kadhaa, vikosi vya Ukraine vilikuwa ndani ya kilomita kadhaa za mpaka wa Russia katika eneo la Kharkiv Jumatano asubuhi, chanzo kimoja cha jeshi la Ukraine kimeliambia shirika la habari la ROITA.
Ofisi ya rais wa Ukraine imesema vikosi vya Russia vilisukumwa taratibu nje ya Kharkiv, ingawa Kyiv haijathibitisha taarifa chache ya kusonga mbele katika eneo, na imeamua kuendelea kuchukua tahadhari.
Wakati huohuo bunge la Marekani lilidhinisha msaada mpya wa dola bilioni 40 kwa ajili ya Ukraine hapo jana, huku wabunge wakiunga mkono ombi la Rais wa Marekani Joe Biden kuashiria dhamira ya pande mbili ya kuzuiya uvamizi wa umwagaji damu wa rais wa Russia Vladmir Putin uliodumu takriban miezi mitatu.
Msaada huo utaliwezesha jeshi la Ukraine katika maswala ya kijeshi na uchumi, kuwasaidia washirika wa kikanda, kuongeza silaha ambazo imesafirisha nje ya nchi na kutoa dola bilioni tano kushughulikia uhaba wa chakula duniani unaosababishwa na vita katika taifa la Ukraine ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mazao mengi .
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Jumanne anaamini hakuna nafasi ya karibuni kufikia makubaliano ya amani au nafasi zozote za haraka za kusitishwa mapigano katika mzozo Ukraine.
Katibu Mkuu anaeleza: “ Ni wazi kwetu kwamba wakati huu hakuna nafasi ya haraka ya makubaliano ya amani au nafasi ya haraka ya kidunia katika kusitisha mapigano kwa hiyo tunazingatia zaidi juhudi za kidiplomasia katika maeneo mawili.
Kwanza, kuwezesha hali ya kuwahamisha na msaada wa kibinadamu katika eneo na makubaliano ambayo yalifikiwa na UN , kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu kufanya kazi pamoja, ambayo nadhani pekee ni jambo la kihistoria na kuwa na uwezo wa kushirikiana na mamlaka za Moscow na Kyiv kuruhusu kuhamishwa raia kutoka Azovstal huko Mariupol na wengine wachache kutoka mji wa Mariupol wameonyesha kuwa bado kuna mengi tunaweza kufanya kwa ajili ya diplomasia kuokoa maisha na kuboresha hali ya kibinadamu kwenye mzozo.”