Msemaji wa NEC alitangaza Jumapili kuwa imemwandikia barua mgombea huyo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kuikashifu NEC kwamba itaiba kura zake, pamoja na madai ya kwamba mgombea urais wa CCM, John Magufuli atakutana na wakurugenzi wa halmashauri hivi karibuni.
Lissu amedai kuwa hatohudhuria suala lolote linalohusiana na kampeni zake.
Lissu ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter, ikiwa zimepita saa kadhaa tu tangu NEC, ilipotoa tamko la kwamba malalamiko hayo yanayohusu mwenendo wa kauli zake wakati wa kampeni .
“Sijapokea malalamiko yoyote juu ya jambo lolote linalohusiana na kampeni za uchaguzi mkuu huu kutoka NEC, sitarajii kuacha kampeni ili kuitikia wito wa mitandaoni wa mtu yeyote,” ameandika Lissu.
Jumapili Septemba 27, 2020, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Charles Mahera, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Arusha, alisema kuwa Lissu alitoa tuhuma hizo kwenye mikutano yake ya kampeni mjini Musoma kati ya Septemba 25 na 26 mwaka huu.