Trump anavyoikosoa VOA, ushahidi tosha ni chombo huru cha habari

Rais Donald Trump akihojiwa na Mwandishi wa VOA Greta Van Susteren June, 12, 2018, Singapore.

Kwa Sauti ya Amerika (VOA) mtendaji mkuu wa habari ambaye alifanya maamuzi mazito, habari ya kipekee na ilikuwa si ya kawaida kuiacha ipite tu.

Siku 10 tu baada ya mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani ambayo yaliua Wamarekani 2,977 na kujeruhi wengine kadhaa, mshirika wa karibu sana wa Osama bin Laden na mlinzi wake nchini Afghanistan, kiongozi Mullah Omar -- alifanya mahojiano maalum na Idhaa ya Pashto ya VOA.

Myrna Whitworth, kaimu mkurugenzi wa Sauti ya Amerika wakati huo, aliwatuma waandishi wawili wa habari kufanya mahojiano kwa njia ya simu na kiongozi wa Taliban ambaye alimruhusu bin Laden, mpangaji mkuu wa mashambulizi ya 9/11, kuwa na makazi nchini Afghanistan.

Lakini maafisa wa utawala wa Bush “waliheshimu haki ya shirika hili kuripoti bila ya upendeleo,” maafisa hawakutaka VOA ifanye “mambo ambayo tulidhani yatakuwa ni faraja kwa adui,” Richard Boucher, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wakati huo, alisema katika mahojiano ya karibuni.

Rais George W. Bush akiongea katika sherehe za miaka 60th ya Sauti ya Amerika (VOA) Februari, 25, 2002, Ofisi za VOA Washington, DC.

VOA, ambayo inafadhiliwa na serikali kuu, ni shirika la kimataifa la utangazaji, linatoa huduma kupitia zaidi ya lugha 40 kwa watu karibu milioni 280 kwa wiki. Lina historia ambayo inaanzia tangu vita vya pili vya dunia na ina mamlaka kutoka katika bunge kuripoti habari kwa kina bila ya kuelemea upande wowote.

Lakini mivutano kati ya White House na VOA imekuwa ni jambo la kawaida kwa miongo kadhaa, kiasi kikubwa kwa sababu ya hali isiyo ya kawaida ya kuwa na uhuru kiasi - na mara nyingine kutumia nguvu zaidi - shirika hili la habari linafanya kazi ndani ya himaya kubwa ya urasimu wa serikali kuu.

Rais Barack Obama akihojiwa na mwandishi wa VOA Andre DeNesnera White House

Mwezi uliopita, Rais Donald Trump aliungana na baadhi ya viongozi waliomtangulia ambao walielezea kutopendezwa na ripoti za VOA -- lakini kwa nguvu isiyo ya kawaida na uchangamfu.

“Kama ungesikia kile ambacho kinatoka Sauti ya Amerika, kinachukiza. Mambo, ambayo wanasema yanachukiza kwa nchi yetu,” Trump amesema wakati akiongea na wana habari kuhusu virusi vya corona kwenye eneo la Rose Garden mnamo April 15.

Malalamiko ya Trump kimsingi yalihusu masuala mawili: Kwanza, kwamba VOA ilitumia takwimu zisizo za kweli za China kuhusu maambukizi ya virusi vya corona na vifo nchini China katika ripoti zake -- shutuma ambazo zimepingwa vikali na taasisi ya habari.

Pili, rais alikuwa amekasirishwa kwamba ameshindwa kuhakikisha mkuu mpya aliyemteua kuongoza taasisi kuu ya VOA - U. S Agency for Global Media - kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili kwasababu ya vikwazo vya wademokrat kumthibitisha katika baraza la Senate.

Trump awali alilalamika juu ya ukosefu wa udhibiti wa chombo cha habari ambacho kinamilikiwa na serikali na kinaashiria thamani yake na ile ya wafuasi wake. Novemba mwaka 2019, Trump alipendekeza kwamba Marekani ni vyema iwe na chombo kinachoendeshwa, kinachosambaza habari ulimwenguni ili kukabiliana na kile alichokiita habari ambazo ‘si haki” na “za uongo” kutoka CNN na kuionyesha dunia jinsi nchi hii ilivyo ‘nzuri.”

Hata hivyo, kama mahojiano ya Mullah Omar na mifano mingine inavyoonyesha, Trump si rais wa kwanza kukosoa ripoti za VOA. Hiyo ni kwa sababu wakati taasisi ya habari kwa kawaida inaongozwa na mtu anayeteuliwa na White House, habari zinazofanywa na waandishi waliobobea katika taaluma hiyo wanatakiwa kisheria kutoelemea upande wowote.

Mabadiliko ya Uhariri katika Shirika la Utangazaji la Serikali

White House na Wizara ya Mambo ya Nje wamekataa ombi la VOA kuelezea zaidi juu ya ukosoaji wa rais uliotangazwa katika televisheni au katika shutuma tofauti ambazo zimeelezewa kwa kina katika kijarida cha White House mapema mwezi huu, ambapo iliishutumu VOA kwa kukuza propaganda za wachina katika matumizi yake ya takwimu wakati wa janga la virusi vya corona.

Mkurugenzi wa VOA Amanda Bennett alilipinga dai hilo na kusema shirika “linajitahidi kuripoti bila ya kupigia debe habari ya upande wowote.”

Kwa hakika, VOA ilielezea udhaifu wa China kwa habari zisizo za kweli karibu mara 20, kwa mujibu wa Kamati ya Wanahabari, kundi ambalo linatetea uhuru wa habari.

Rais John Kennedy alipotembelea Sauti ya Amerika Mwaka 1962.

Mwelekeo huu wa uhariri siku zote haukuwa ni sera ya VOA. Baada ya shirika hili kuundwa mwaka 1942 kupambana na propaganda za Nazi kwa habari maalum, katika miongo ya kwanza ya VOA kuripoti ambapo ilikuwa ni kwa idhini ya wahusika katika serikali.

Wakati wa enzi ya Kennedy mzozo wa kombora la Cuba mwaka 1962, VOA kimsingi ilikuwa ikifanya kazi “chini ya uangalizi wa serikali,” amesema Nicholas Cull, profesa wa diplomasia ya umma katika chuo kikuu cha Southern California Annenberg katika chuo cha elimu ya Mawasiliano na Uandishi wa Habari na mwandishi wa kitabu “The Cold War na Idara ya Habari ya Marekani.”

“Kulikuwa na afisa utawala aliyepelekwa VOA kutoka idara ya habari ya Marekani,” amesema Cull. “Alikuwa anaidhinisha kila habari.”

Mwelekeo huo ulivurugika wakati wa kashfa ya Watergate ambayo ilipelekea Rais Richard Nixon kujiuzulu mwaka 1974. Cull amesema kwamba waandishi wa habari wa VOA ambao walisisitiza kutoa picha kamili kuhusu uchunguzi kuhusiana na shutuma kuwa rais alifanya makosa walipata upinzani kutoka kwa maafisa wa USIA ambao walitaka habari chanya zaidi.

Waandishi walitaka suala la Watergate liwe ni “somo la uraia litangazwe kuonyesha kwamba nguvu ya Marekani haiko kwa rais kwamba hajawahi kufanya kosa, lakini uwezo wa Bunge kusahihisha kosa hilo kupitia mchakato unaostahili,” amesema Cull. Mwishowe, muafaka ulifikiwa kwamba kila wakati kama kuna habari mbaya kuhusu rais, habari nzuri ni vyema itolewe pia.

“Hii ilipelekea aina fulani ya matangazo ya ajabu,” amesema Cull. “Walikuwa wakisema, katika habari hivi leo Rais ametajwa kuwa ni mhusika ambaye hatashtakiwa katika mgogoro wa Watergate… na Mke wake Bi Nixon amefungua shule mpya ya watoto hapa Washington DC.”

Shirika la Habari lilizuiliwa kuonyesha upendeleo

Mnamo mwaka 1976, Bunge na watendaji wa VOA waliazimia kuwa shirika hilo linahitaji mamlaka ya wazi ya uhariri kuhakikisha kwamba wanadumisha uaminifu wao kwa wasikilizaji wa nje. Bunge liliandika rasimu ya Muongozo, ambayo inasema VOA lazima itangaze habari za uhakika; iwe na habari ambazo zinawakilisha jamii ya wamarekani wote; na kutoa maelezo ya wazi na majadiliano kuhusu sera za Marekani.

Muongozo Maalum wa VOA

  • Maslahi ya taifa la Marekani yanafikiwa kwa kuwasiliana moja kwa moja na watu ulimwenguni kupitia radio. Kufanikisha hilo, Sauti ya Amerika lazima iweze kuwavutia na kuheshimika na wasikilizaji wake. Kwa hivyo misingi hiyo ndio itasimamia matangazo ya Sauti ya Amerika :

  • VOA itakuwa siku zote ni chanzo cha kutegemewa na kuaminika cha habari. Habari za VOA zitaendelea kuwa sahihi, bila kuegemea upande wowote na za kina.

  • VOA itawakilisha taifa la Marekani, na siyo tabaka mmoja tu ya jamii ya Wamarekani, na kwa hiyo itaendelea kutoa habari za pande zote husika na za kina zinazoelezea fikra muhimu za Marekani na taasisi zake.

  • VOA itawasilisha sera mbalimbali za taifa la Marekani kwa ufasaha na inavyopaswa, na pia italeta mijadala mbalimbali inayochunga haki za wengine na maoni juu ya sera hizo.​

Gerald R. Ford
Rais wa Marekani

Imesainiwa Julai 12, 1976
Sheria ya Umma 94-350​

Richard Stengel, mhariri wa zamani wa jarida la Time na waziri mdogo wa zamani wa Mambo ya Nje kwa Masuala ya Diplomasia katika utawala wa Obama, amesema uhuru huu unaitofautisha VOA na baadhi ya washindani wake. Utaratibu wa kihariri kuhusu shirika ulifafanuliwa zaidi katika sheria mwaka 1994 na mwaka 2016, ambayo ilielezea hatua maalum kuwakinga waandishi wa habari kutokana na ushawishi wa kisiasa na kulitaka shirika kuheshimu “viwango vya juu vya uandishi wa utangazaji” wakati wakiendelea kuwa na msimamo thabiti “kuhusu malengo ya sera ya mambo ya nje ya Marekani.”

“VOA si chombo cha utangazaji cha serikali ya Marekani kama ilivyo TV katika nchi zenye utawala wa kiimla ambazo zinatakiwa kuonyesha malengo ya sera za mambo ya nje au misingi ya nchi husika. Si kama inavyofanya Korea Kaskazini, au China inavyofanya, au Cuba inavyotenda, au sehemu kama hizo. Ni chombo huru cha utangazaji na kwa sababu hiyo VOA inafuatiliwa na kupendwa na mamilioni ya watu kote duniani,” Stengel amesema.

Rais Ronald Reagan akitoa hotuba yake ya kila wiki kupitia radio ya Sauti ya Amerika

Shirika la Utangazaji la Marekani, watendaji wanaidhinishwa na White House

Wakati wa waandishi wa habari wa VOA walihitajika kuripoti habari za kweli, shirika chini ya mamlaka ya utendaji, ina madaraka ya kumteua Mtendaji Mkuu wa shirika mama la VOA, U.S Agency for Global Media.

USAGM inasimamia idara tano ambazo zinapata ufadhili wa serikali kutoa huduma za mitandao ya habari kwa umma ambapo wanaripoti habari kwa nchi ambako vyombo vya habari vinakumbwa na masharti makali. Mtendaji Mkuu wa USAGM, pamoja na bodi ya watendaji wa habari na watalaamu wa masuala ya kimataifa wasioelemea upande wowote, wanateua wakuu wa mitandao ya habari, ikiwa pamoja na VOA.

Trump alimteua Juni 2018 Michael Pack, mtengeneza filamu mconservative na mkuu wa habari, kama mtendaji mkuu wa USAGM.

Seneta Mdemokrat Bob Menendez wa New Jersey hivi karibuni aliandika barua White House akisema Pack bado hajajibu maswali ya kamati kuhusu shutuma za biashara yake, taarifa za zamani za kodi ya mapato, na kudai “mazingira mabaya” ya kuondoka kwake katika kazi yake ya zamani.

Msemaji wa Pack aliiambia VOA kuwa hataki kutoa maoni kwa habari hiyo, kutokana na kuendelea kwa utaratibu wa uteuzi wake.

Clifford May, mkuu wa taasisi ya Ulinzi wa Demokrasia, amesema ukosoaji wa Trump kwa VOA unastahili kwasababu ya kukasirishwa kwake juu ya kutoidhinishwa kwa mgombea aliyemteua.

May alielezea sifa za Mkurugenzi wa VOA, Amanda Bennett kama ni mtu aliyetoka katika utawala wa Rais Mdemokrat Barack Obama, ambaye alishindwa kuelezea kwa kina sera za utawala wa Trump kwa dunia.

“Hilo ni vyema lielezewe kwa VOA -- kama si huko, wapi kwingine? Hiyo haimaanishi kwamba hakuwezi kuwepo maoni ya wazi, au ukosoaji wa rais pia. Mambo yote hayo yanaweza kuwepo katika kuleta uwiano. Inataka mwandishi wa habari mzuri kufanya hivyo,” May amesema. “Ni dhahiri kwamba utawala huu unadhani hilo halifanywi kwa usahihi na wale ambao wana mamlaka.”

Bennett, mtendaji na mhariri wa zamani wa Bloomberg News na Philadelphia Inquirer, alipewa wadhifa wa mkurugenzi wa VOA mwaka 2016 na ameendelea kuongoza shirika hilo mpaka kuingia kwa utawala wa Trump.

Rais Bill Clinton akizungumza kutoka Sauti ya Amerika, Washington, DC, Octoba 24, 1997.

Wakati wa mgogoro wa mwaka 2001 uliohusu mahojiano na Mullah Omar, waandishi wa habari wa VOA zaidi ya 100 walizungumza, walitia saini waraka kulisihi shirika hilo kupinga shinikizo. VOA iliishia kurusha hewani vipande vya mahojiano na ilitoa taarifa kutetea hilo kwa wakosoaji wake. “Watu wa Afghanistan wanatusikiliza kwasababu wanatuamini, na sisi tunawaambia habari zote,” sehemu ya taarifa ilisema hivyo.

Boucher, ambaye hivi sasa ni profesa wa masuala ya mambo ya nje katika chuo kikuu cha Brown, amesema kwamba pande zote baadaye “ziliachana” na malumbano. Chini ya wiki mbili baada ya mahojiano hayo kurushwa, Whitworth alihamishwa kutoka katika wadhifa wake kama kaimu mkurugenzi wa VOA na nafasi yake kuchukuliwa na mteuliwa wa White House, Robert R. Reilly.

“Shinikizo halikuwa dhahiri kabisa lakini walieleza bayana kwamba sikutakiwa kuwa na jukumu katika maamuzi ya kiuhariri,” amesema Whitworth, ambaye ana ujuzi kama mwandishi wa habari katika shirika hilo, na siyo mteuliwa wa kisiasa. Aliamua kustaafu mapema.

Shirika la Serikali la Utangazaji ambalo linapitia katika mivutano ya kisiasa

Vipindi vya siasa za mgawanyiko nchini Marekani, kama vile kumshtaki rais kutaka kumuondoa madarakani au vita, kunaweza kuiweka VOA katika nafasi ngumu, amesema Lata Nott wa Freedom Forum. Lakini hizo pia anasema ni nyakati ambazo shirika la utangazaji linajenga uaminifu kwa wasikilizaji wake.

“Ukweli ni kwamba taasisi zetu za habari ambazo zinafadhiliwa na serikali kuu haziendeshwi na serikali, lakini kuwa huru ni jambo muhimu sana,” Nott amesema.

“Ni kawaida kwa serikali kusema tunalipia hili, tunataka habari zetu nzuri zielezewe,” amesema Profesa Cull wa USC.

“Ni kawaida kwa waandishi wa habari kusukuma na kusema maadili ya uandishi yanahusu habari kuwa na pande zote mbili, na iwe na ufanisi, lazima tuonyeshe uaminifu.”

Mtangazaji wa iliyokuwa Idhaa ya Kijerumani ya Sauti ya Amerika Robert Bauer

Tangu ilipoanzishwa mwaka 1942 kupambana na propaganda ya WaNazi na pamoja na kuwepo baadaye sheria zinazolinda uhuru wa uamuzi wa wahariri katika chumba cha habari cha VOA, shirika hili limepigania changamoto zake mbalimbali katika kuendeleza uhuru wake. Hii hapa ni mifano mbalimbali :

  • Mwanzoni mwa miaka ya 60, VOA haikuweza kutangaza juu ya mgogoro wa makombora ya Cuba bila ya ruhusa ya Shirika la Habari la Marekani (USIA), wakati huo likiwa ni msimamizi wake.

  • Wakati wa kuripoti kashfa ya Watergate iliyopelekea Rais Richard Nixon kujiuzulu mwaka 1974, VOA ilikinzana na maafisa wa USIA waliotaka habari hizo zipewe sura nzuri. Makubaliano yalifikiwa kuwa kila wakati habari mbaya itakapo ripotiwa juu ya Nixon, habari yenye kumwonyesha vizuri pia iripotiwe wakati huo huo.

  • Wakati wa Utawala wa George H.W. Bush, USIA ilijaribu kuzuia mahojiano ya VOA na Fang Lizhi, mpinzani huyo wa China alipokuja Marekani mwaka 1990. Fang alikuwa amekimbilia Ubalozi wa Marekani mjini Beijing na sehemu ya makubaliano ya kumruhusu kuondoka China ilikuwa Washington haitatumia habari ya mpinzani huyo kwa maslahi yake.

  • Tukio kama hilo lilitokea pia mwaka 1997 wakati utawala wa Clinton ulipofanikiwa kuachiwa huru kwa Wei Jingsheng na kujaribu kuzuia kutangazwa hewani mahojiano aliyofanya na VOA kwa kuhofia kuwa itazuia siku za usoni kuachiwa kwa wapinzani wengine.

  • Wiki kadhaa baada ya shambulizi la Septemba 11, Wizara ya Mambo ya Nje chini ya utawala wa George W. Bush ilijaribu kuzuia VOA kutangaza mahojiano maalum na kiongozi wa Taliban Mullah Omar, aliyekuwa amemruhusu Osama bin Laden kuishi Afghanistan.

  • Mijadala kuhusu “jukumu la VOA baada ya shambulizi la Septemba 11” iliendelea baada ya VOA kupeperusha sehemu ya mahojiano hayo. Baadhi ya maafisa katika Utawala wa Barack Obama walieleza kero lao kwamba ripoti ya VOA ilikuwa haiakisi sera ya mambo ya nje ya Marekani dhidi ya misimamo mikali yenye uvunjifu wa amani.

Vyanzo vya habari : Mahojiano ya waandishi wa VOA; Nicholas Cull, The Decline and Fall of the United States Information Agency: American Public Diplomacy, 1989 - 2001, 2008; Alan L. Heil, Jr, Voice of America - A History, 2003.