Kuzinduliwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuleta manufaa mbalimbali katika kukuza biashara na uchumi nchini humo kutokana na treni hiyo kutarajiwa kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam na kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Rais Samia amesema treni hiyo itaongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam kutokana na treni hiyo kuwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa kwa wakati mmoja mpaka kufikia shehena ya tani milioni 17 kwa mwaka na hivyo kurahisisha ufanyaji wa biashara na kupunguza msongamano wa mizigo.
“Tunatarajia kuwa reli hii itaongeza ufanisi wa bandari zetu hususani bandari ya Dar es Salaam kwa kuondosha mizigo kwa haraka kutokana na reli hii kuhudumia shehena ya mizigo ya tani 17 million kwa mwaka,” amesema Rais Samia.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kwa kipindi cha muda mfupi mpaka kufikia July 28, 2024.Treni hiyo ya kisasa ilikuwa imekwisha safirisha abiria wapatao 28,600 na kukusanya kiasi cha fedha za Kitanzania Shilingi Milioni 744 toka kuanza kwa safari hizo.
Hata hivyo baadhi ya Wachumi wameonyesha wasiwasi juu ya hitilafu ya umeme iliyojitokeza wakati wa safari ya majaribio iliyopelekea Treni kusimama kwa muda wa masaa mawili na baadae Shirika la Reli Tanzania wakatoa ripoti ya awali kuwa hitilafu hiyo ilisababishwa na Ngendere na Ndege aina ya Bundi.
Suala ambalo Dkt Ntui Ponsian Mhadhiri kutoka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza, amesema Shirika la Reli la Tanzania linapaswa kujiepusha na utoaji wa kauli kama hizo kwakuwa kauli hizo zinaweza kupelekea wateja na wananchi kupoteza imani na huduma zinazotolewa na shirika hilo.
“TRC wanapaswa wajiepushe sana na kauli kama zile kwasababu zinaleta taswira watu kutaka kujiuliza kwamba wakati tunaandaa mradi huu na kuweka nyaya za umeme hatukuona tumbili Bundi au ndege wengine pia taswira kwa watumiaji wanaweza wakaona kwamba safari hazina uhakika kama unaweza ukakaa masaa mawili porini kwasababu ya tumbili tu je kikitokea kingine si unaweza ukakaa porini siku nzima.” Amesema Ponsian.
Aidha Rais Samia amewatoa wasiwasi wa kukosa abiria wawekezaji waliowekeza katika sekta binafsi upande wa usafirishaji kwa njia ya Mabasi kwa kutoa ruhusa kwa wawekezaji hao kutafuta namna ya kuingia ubia na shirika la Reli Tanzania kutengeneza mfumo utakaowawezesha abiria kusafiri kwa kutumia tiketi moja kuunganisha safari katika Mabasi yanayokwenda katika mikoa mingine.
“Reli hii pia inaweza kuwa na fursa kwa wadau wa sekta binafsi kwa mfano wasafirishaji wa abiria wanaweza kuingia ubia na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wakawa na tiketi moja ambayo mtu atapanda treni na akishuka anajua atapanda basi fulani kwenda sehemu fulani kwa tiketi hiyo hiyo moja,” ameongezea Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa mpaka kukamilika kwa Mradi huo wa Reli ya kisasa ya umeme (SGR) kunatarajia kuigharimu serikali ya Tanzania jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 10 ambazo ni sawa na Trilioni 23.3 za Kitanzania na hivyo amewataka Watanzania kuulinda mradi huo kwa wivu mkubwa.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.