Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 06:14

Tume huru ya uchaguzi Tanzania yaanza kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura


Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima, baada ya kuapishwa March 19, 2021. Picha na AFP.
Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima, baada ya kuapishwa March 19, 2021. Picha na AFP.

Tume huru ya uchaguzi Tanzania wiki hii inaanza kazi ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura huku vuguvugu la kuelekea katika uchaguzi mkuu mwakani na wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu likianza kupanda miongoni mwa vyama vya siasa.

Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora ndiyo itayokuwa ya kwanza kuanza kasi ya uboreshaji wa daftari hilo hapo siku ya Jumamosi na baadaye kazi hiyo inatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine, ikiwalenga wale waliofikisha umri wa kupiga kura yaani miaka 18 na ambao walikuwa bado hawajaandikishwa.

Kwa sasa Tanzania inajiandaa na uchaguzi mkuu hapo mwakani uchaguzi ambao tayari umeanza kuvishughulisha vyama vya siasa vinavyoendelea kutumia majukwaa ya kisiasa kukosoana.

Uchaguzi wa mwakani unatarajiwa kutanguliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na utasimamiwa na Tamisemi huku tume hiyo ya uchaguzi ikiendelea na jukumu la kusimamia uchaguzi mkuu.

Katika mahojiano maalumu na VOA, mkurugenzi wa tume hiyo Ramadhani Kailima anasema uboreshaji wa daftari la kudumu unafanywa kwa awamu mbili katika kuelekea kilele cha uchaguzi wenyewe.

Demonstrators in Dar es Salaam calling for constitutional change
Demonstrators in Dar es Salaam calling for constitutional change

Ingawa vyama vya upinzani vimekuwa vikihimiza haja ya kupatikana kwa katiba mpya kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, hata hivyo vinaamini viko katika mkondo salama wa kukitikisa chama tawala CCM.

Uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 umekuwa ukikosolewa vikali na upinzani kwa madai ya matokeo yake kuchakachuliwa ikiwemo baadhi ya wapinzani pia kuandamwa na vyombo vya dola.

Kutokana na mazingira yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi huo uliopita, baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanasema kuna haja ya kuwa na duru ya maridhiano ili kujenga uwanja wa kuaminiana kuelekea katika uchaguzi huo.

Akizungumzia hatua hiyo, Waziri mkuu wa zamani na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko katiba, Joseph Warioba anasema ni muhimu pande zinazohusika na uchaguzi kutembea katika misingi ya haki na ukweli ili yale yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita yasijirudie tena.

Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi wakisheherekea ushindi wakati wa uchaguzi wa Rais Oktoba 30, 2020.
Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi wakisheherekea ushindi wakati wa uchaguzi wa Rais Oktoba 30, 2020.

Tume huru ya taifa ya uchaguzi tayari imekamilisha mchakato wa awali wa kupokea baadhi ya vifaa vya kupigia kura ikiwemo mashine ya BVR. Hata hivyo baadhi ya vyama vya siasa vinashutumu hatua hyo vikisema havijashirikishwa katika hatua hiyo.

Ama, vyama hivyo vinakosoa kuhusu kuchelewa kutolewa kwa kanuni zinazosimamia uchaguzi vikisema kuchelewa kwake kunaweza kusababisha hali ya sintofahamu.

Lakini mkurugenzi wa tume, Kailima amepuuza hja mbali mbali akisema vyama hivyo vinapaswa kutembea katika kweli.

Wakati ambapo mamlaka husika bado haijatangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mbali na kuanza tu kwa kampeni ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, vyama vya kisiasa vimekuwa vikizunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi kuzungumza na wanachama wao pamoja na kuwavutia wapiga kura wapya.

Forum

XS
SM
MD
LG