Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:59

Uchaguzi wa Rwanda kufanyika leo


Rais wa Rwanda Paul Kagame Jumamosi amekamilisha kampeni yake siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Jumatatu.

Kiongozi huyo anakabiliana na wapinzani wawili ambao wamedai kuwa amesalia madarakani kwa muda mrefu zaidi. Hata hivyo Kagame amesema kuwa wafuasi wake wanataka awanie kwa muhula mwingine.

Akizungumza na wanahabari baada ya kukamilisha mkutano wake wa mwisho wa kampeni, Kagame alisema kuwa vipaumbele vyake kwenye taifa ambalo amekuwa akiongoza tangu 2000 havijabadilika.

"Kipaumbele cha kwanza ni kupiga hatua iwezekanavyo kuelelekea kwenye usalama na uthabiti wa nchi yetu, maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kukuza taifa letu kuelekea ustawi."

Huu utakuwa muhula wa nne iwapo Kagame atashinda kwenye uchaguzi wa wiki hii.

Kiongozi huyo anamenyana na wagombea wengine wawili akiwemo Frank Habineza wa chama cha Democratic Green ambaye pia alishindana naye 2017, ambaye anasema anadai kuwa Kagame amesalia madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Habineza aliambia VOA kuwa amefanya kampeni kamilifu kwenye karibu wilaya 30 kote nchini, na kwamba wapiga kura wakati huu wana Imani kubwa naye.

"Nawapa matumaini kwamba baada ya miaka 30, tunahitaji kuona mambo kwa mtazamo tofauti, program tofauti za kisiasa, mawazo tofauti na maoni tofauti. Hatutaharibu mema ambayo yamefanywa awali, lakini tunataka kuwapa matumaini mema, na kesho bora zaidi."

Kagame wakati akizungumza na wanahabari alisema kuwa hakutaka kuwa rais lakini chama chake kilisisitiza kuwa aingie kwenye kinyang’anyiro cha mwaka 2000. Miongo kadhaa baadaye, wafuasi wake wanamuomba aendelee kuwania.

"Kila siku naulizwa unaondoka lini ? Hawa watu walionifanya rais wanasisitiza kuwa wanataka niendelee kuwa rais. Mtu mwingine anasema hapana, umedumu sana. Mimi huchanganyikiwa. Nafikiri siyo haki."

Kagame mwenye umri wa miaka 66 anatarajiwa kushinda kwa urahisi. Sababu moja kuu kulingana na wakosoaji wake ni kwamba alizima upinzani.

Kwa wengine, wanasema kuwa ni kutokana na namna alivyoendesha taifa hilo la Mashariki mwa Afrika kuelekea kwenye amani tangu mauaji ya kimbari ya 1994, pale ambapo takriban watu 800,000 wengi wakiwa wa Tutsi na wa Hutu wenye msimamo wa wastani waliuwawa na wa Hutu wenye msimamo mkali.

Kuna baadhi ya wagombea waliozuiliwa kushiriki uchaguzi wa mwaka huu na tume ya kitaifa ya uchaguzi kutokana na sababu kadhaa.

Mmoja alikuwa mkosoaji mkubwa wa Kagame Diane Rwigara, ambaye tume hiyo ilisema kuwa hakutoa rekodi ya uhalifu na pia hakupata sahihi za kutosha kutoka kwa wafuasi wake.

Forum

XS
SM
MD
LG