Tanzania : Magufuli asisitiza ujenzi wa mradi wa Stiegler's Gorge hautaathiri mazingira

Stiegler’s Gorge nchini Tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli, amezindua Ijumaa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika mbuga ya wanyama ya Selous.

Rais Magufuli amesisitiza kwamba mradi huo hautaathiri mazingira na badala yake unaimarisha ukuaji wa uchumi kupitia ujenzi wa viwanda.

Amesema asilimia tatu pekee ya sehemu hiyo ya mbuga ya wanyama, yenye ukubwa wa kilomita 50,000 mraba, itatumika kwa ujenzi huo.

Mfuko wa wanyamapori ulimwenguni unasema mradi huo wa umeme utaathiri maisha ya watu 200,000 ikiwemo wakulima na wavuvi katika mto Rufiji.

Mbuga ya Seluu, ni makao ya ndovu, vifaru weusi na mbwa mwitu.

Mradi huo uko katika eneo la mto Rufiji, ambayo ni urithi wa ulimwengu.

Tangu rais atangaze kujengwa kwa mradi huo kumekuwapo pingamizi za watetezi wa mazingira wakitahadharisha athari hasi kwa hifadhi ya wanyama.

Watetezi hao wameeleza hilo ni janga kwa uharibifu usiyoweza kukadirika kwa hifadhi kubwa kuliko zote ya wanyama ya Selous kwa Afrika nzima.

Tangu mwaka 1982, Selous ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa ni eneo la Urithi wa Ulimwengu, lenye thamani kwa ulimwengu chini ya Mkataba wa UNESCO uliyosainiwa na nchi 193.

Kujenga bwawa la kuzalisha umeme lenye urefu wa kilomita 100 na kilomita 25 kwa upana itakuwa ndiyo mwanzo wa kuiua hifadhi hiyo ya Selous ambayo ni sehemu ya kipekee ya maisha salama kwa wanyama.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2,100 za umeme na kuongeza mara tatu kiwango cha umeme nchini Tanzania.

Tanzania inakumbana na matatizo makubwa ya umeme, asilimia 10 pekee ya familia ikiwa ndiyo iliyo na nguvu za umeme.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington, DC.