Takwimu za Shirika la New Frontier zinaonyesha Tanzania ni nchi ya tano ya Kiafrika, ambayo raia wake milioni 3.6 wameeleza kuwa wanatumia bangi, limeripoti gazeti la The Citizen, Jumatatu nchini Tanzania.
Katika EAC Tanzania inaongoza nchi nyingine mbili zenye idadi kubwa ya watu ambazo ni Kenya ambayo inawatumiaji milioni 3.3 na imeorodheshwa kuwa nafasi ya sita katika utumiaji bangi Afrika na Uganda yenye idadi ya watumiaji wa bangi milioni 2.6 ikiwa imechukuwa nafasi ya nane katika utumiaji bangi Afrika.
Watumiaji wa juu kabisa wa bangi Afrika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni Nigeria ikiwa na watumiaji wa bangi milioni 20.8, Ethiopia inawatumiaji milioni 7.1, Misri watumiaji milioni 5.9 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa nafasi ya nne na watumiaji milioni 5.
Kwa mujibu wa utafiti huo, Nigeria ina idadi kubwa ya watumiaji wa bangi, ambapo asilimia 19.4 ya wakazi wake wenye umri wa miaka 15 na zaidi ambao wametumia bangi mwaka mmoja uliopita.
Mwaka 2018, Afrika imesajili matumizi ya bangi yenye thamani ya kustaajabisha ya paundi bilioni 37 inayotumika barani humo.
Uchambuzi wa hivi karibuni wa Shirika la New Frontier Data unaonyesha mahitaji makubwa ya bangi ambapo zaidi ya watu wazima milioni 260 duniani wanatumia bangi angalau mara moja kwa mwaka.
Jumla ya kiwango cha fedha cha kustaajabisha kununua bangi kila mwaka ni dola za Marekani bilioni 344.