Rais alisema hayo katika hafla ya kuwaapisha; mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Venance Mabeyo na wengine aliowateua kuwa mabalozi nchi za nje.
“Katika vita hii ya madawa ya kulevya, hakuna cha mtu aliye maarufu, hakuna cha mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri au mtoto wa fulani ambaye akijihusisha ataachiwa,” Rais ameonya.
“Hata ingekuwa mke wangu Janet, akijihusisha akamatwe tu na kushtakiwa,” alisema.
Madhara ya mihadarati kitaifa
Rais amesema kuwa madhara ya madawa ya kulevya yamelifikisha taifa mahali pabaya.
“Si siri sote tuliopo hapa tunafahamu madawa ya kulevya yanapoteza nguvu kazi ya watanzania,” amesisitiza.
Mapema Jumatatu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda alitoa onyo kwa wazazi na watendaji wa mitaa mjini humo na kuwakumbusha wajibu wao katika kutoa taarifa za uhalifu.
Atoa siku kumi
“Nasema baada ya siku kumi tukimkamata mtu ana madawa ya kulevya mtaani kwako na wewe hujajishughulisha tunaweza kuamini unahusika na jambo analolifanya linalo kunufaisha.”
Pia Makonda amesema: “La pili ninawapa siku 10 wazazi, kila mmoja ahakikishe anajua mtoto wake kama anatumia madawa au hatumii.”
Wakati amri hii ikitolewa polisi tayari wamesha wakamata watu zaidi ya 100 kwa tuhuma za kuhusika na madawa ya kulevya jijini Dar es Salaam.
Kamanda Sirro
Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi kanda maalum Dar es Salaam Simon Sirro amesema baadhi ya hao waliokamatwa ni pamoja na Omari Micheni na Wema Sepetu.
“Baada ya kumhoji Wema na kuwahoji wenzake wanaotumia madawa hayo na kueleza vizuri. Alikutwa na msokoto wa Bangi na baadhi ya karatasi maalum zinazotumika kufungia bangi,” alieleza Kamanda Sirro.