Tanzania: Hofu yatanda juu ya kasi ya deni la serikali kuendelea kuongezeka kila mwezi

President Samia Suluhu Hassan addresses both Houses in Kenya. Photo Courtesy of State House, Tanzania

Hofu na wasiwasi umetanda  nchini Tanzania kufuatia kasi ya deni la serikali kuendelea kuongezeka kila mwezi kwa kiwango cha dola milioni 544.8.

Wakati huo huo wataalamu wa uchumi wametahadharisha ikiwa serikali haitakuwa na utaratibu mzuri na wenye nidhamu katika matumizi ya fedha wanazokopa itapelekea kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa taifa na mtu mmoja mmoja na pato la nchi kupungua.

Ongezeko la kasi ya deni la taifa limeendelea kuwa gumzo na kuleta mijadala mikali kwa wananchi huku kukiwa hakuna majibu ya kina kuhusu kile kinachoonekana hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu wakati ambapo hata wataalamu wa uchumi wanashangazwa na hali hii.

Profesa Aurelia Kamuzora ambaye ni mtaalamu wa uchumi, katika idara ya uchumi kwenye chuo kikuu cha Mzumbe na mwenyekiti wa baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini Tanzania anaitahadharisha serikali kutumia vizuri pesa walizokopa katika uzalishaji kwa kuhakikisha miradi yote iliyokusudiwa iende mahali palipokusudiwa ili taifa lipate matunda ya mkopo huo na kila mwananchi aweze kunufaika.

Kwa mujibu wa ripoti ya benki kuu inaonyesha hadi kufikia mwezi Oktoba 2022 deni la taifa lilikuwa limefikia Shilingi trilioni 90.35 huku baadhi ya wataalamu wakiona ongezeko hilo ni kubwa kama nchi itashindwa kuzirudisha fedha hizo huenda ikajiingiza katika shida zaidi

Dr Issa Hemedi Mkuu wa idara ya uchumi kutoka chuo kikuu Zanzibar akizungumza na sauti ya Amerika amesema pamoja na faida zinazoweza kupatikana kwa nchi kukopa lakini pia kuna athari nyingi zinaweza kujitokeza hasa madeni yanapozidi kuongezeka kwa nchi zenye ndoto ya kutaka kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo Walter Nguma mchambuzi wa masuala ya kiuchumi kutoka Dar es Salaam amesema iwapo kuna faida kwa nchi kukopa kama tu itaamua kuwa na nidhamu nzuri ya matumizi lakini pia ametahadharisha kuwa madeni yanapoongezeka kwa kasi inaweza kupelekea kupunguza ari ya uchumi wa kujitegemea kwa taifa

Ikumbukwe nchini Tanzania hakujawahi kushuhudiwa ongezeko la deni kubwa kiasi hiki tena katika kipindi kifupi hali ambayo inatajwa kuweza kuiingiza nchi kwenye matatizo ya kiuchumi na kuifanya ishindwe kukopesheka kama asemavyo Mtaalamu wa Uchumi Profesa Aurelia Kamuzora

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania