Wanataka serikali iweke utaratibu wa bajeti za dharura na uwekezaji mzuri katika usimamizi na uzalishaji, wakiwataka viongozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Tangu kuanza kwa mwaka 2022 Watanzania wamekuwa wakishuhudia ongezeko la bei za bidhaa zisizo za kawaida huku maelfu ya familia zikisononeka kwa kushindwa kukidhi mahitaji yao ya msingi ya chakula kutokana na gharama hizo kuwa juu.
Kiongozi wa dini ambaye pia ni mdau wa maendeleo Emmaus Mwamakula anaitaka serikali kuwa tayari kujifunza kutoka katika mataifa yaliyoendelea namna wanavyoweza kupambana na athari mbalimbali zinazo weza kujitokeza.
Anasema hasa katika jambo hili la mfumuko wa bei na kudhibiti bei za bidhaa kupanda kiholela.
Ni dhahiri bei za bidhaa zinapopanda mara kwa mara zinazorotesha kwa kiasi kikubwa harakati za kujikwamua kiuchumi hali ambayo imeonekana kuwaumiza walio wengi hasa wananchi wa vipato vya kati na vya chini.
Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Sweden Dr.Willbrod Slaa katika kutafuta suluhisho juu ya hali hii ameishauri serikali kuwa na usimamizi imara katika uzalishaji na waache kufanya kazi kwa mazoea kwa kutegemea mvua pekee katika shughuli za uzalishaji bali watazame namna bora katika kilimo cha umwagiliaji.
Madhara ya mfumuko wa bei uliopo yanaonekana kila mahali katika nchi hii kutokana na malalamiko yanayotolewa na wananchi na wakazi wa maeneo mbalimbali hali ambayo haijawahi kushuhudiwa na watu walio wengi.
Riziki Mgwali mkazi wa Magomeni Dar es Salaam akizungumza na sauti ya Amerika amesema hali hii ya kupanda kwa gharama za bidhaa zimetikisa kwa kiasi kikubwa utaratibu wa maisha yao ambapo hata bajeti zao kwa sasa zinashindwa kupangika vizuri kutokana na bidhaa hizo kukosa bei elekezi ambapo mara kwa mara gharama hupandishwa.
Emmaus Mwamakula mdau wa maendeleo anashauri katika kudhibiti hali ya bidhaa kupanda kwa kasi Serikali inawajibu wa kuyafanyia kazi maneno ya wataalamu na wadau wa maendeleo kwa kuyachukua kikamilifu mawazo yao na kuyaingiza katika mipango yao kwa vitendo na kuepuka kuiweka mipango yao kwenye karatasi pekee.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.