Tanzania : CAG abaini ukiukwaji wa sheria na maadili

Charles Kichere

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Tanzania (CAG), amezungumzia ukaguzi wa hesabu za mashirika na taasisi za serikali kwa mwaka 2019/2020 ambapo amesema amebaini ukiukwaji mkubwa wa sheria za fedha za umma na kanuni za maadili ya utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Alhamisi CAG Charles Kichere pamoja na mambo mengine, katika ripoti hiyo amebaini matumizi mabaya ya mamilioni ya shilingi, wakati Wizara ya Maliasili na Utalii ilipoendesha matamasha na shughuli za kukuza utalii wa ndani ambapo taratibu za malipo ya fedha hazikufuatwa.

Aidha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali ametoa hati mbaya kwa taasisi kumi, huku taasisi nyingine 81 zikipewa hati zenye mashaka, kutokana na ukaguzi uliofanywa

Kichere amesema kuna taasisi kumi na tatu zimefanya matumizi ya fedha kinyume na bajeti zilizopangwa na kuidhinishwa na bunge, ambazo ni Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA), Wakala wa Barabara (TANROADS), Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, Wakala wa Barabara (TARURA), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe.

Ripoti hiyo ya CAG imekabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAC) Grace Tendega na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali Kuu (PAC) Japhet Asunga, ambao wameahidi kuifanyia kazi na kuishauri serikali hatua za kuchukua.

Hata hivyo CAG ametoa rai kwa taasisi na mashirika ya serikali ambayo yalishindwa kuwasilisha hesabu za kila mwaka kwa ajili ya kutolewa maoni ya ukaguzi kufanya hivyo ili kutimiza takwa hilo la kikatiba