Awatef Adam, mama wa watoto saba mwenye umri wa miaka 43, alikimbia mauaji ya wiki kadhaa katika mji wa Sudan wa El Geneina hadi Chad katikati ya mwezi Juni.
Mama huyo ilimlazimu kumuacha nyuma mtoto mmoja wa kiume na wengine wa kike watatu kwa jamaa na majirani katika jiji hilo na kukimbilia Chad akiwa na mtoto wake mwingine na mabinti wawili.
Alikuwa na matumaini hii ingemhakikishia kwamba baadhi ya watoto wake watanusurika.
Hali Inayowakabili Wanawake na Watoto
Huku akifahamu wanamgambo wa Kiarabu walikuwa wakiwalenga wanaume wa Masalit kwa safari ya kwenda Chad, Awatef Adam alimvisha mwanawe Fayez mwenye umri wa miaka 12 kitambaa kichwani na abaya nyeusi, vazi linalovaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu.
Fayez alipita baadhi ya vituo vya ukaguzi vinavyosimamiwa na RSF bila kutambuliwa.
Lakini walipofika Shukri, kijiji kilicho umbali wa kilomita 10 kutoka mpaka wa Chad, wanaume waliovalia sare za RSF walimtambua Fayez na kumkamata.
Awatef Adam anaeleza yaliyowafika: “Walimpiga kichwani, Walikuwa wakimpiga na rungu la mbao. Niliwaambia wasimpige. Yeye ni yatima. Mara wakanipiga. Nilianguka chini. Kupigwa kichwani kulisababisha mkono wangu kupooza. Walinipiga kichwani. Nilianguka chini. mume wangu alipigwa na nilijaribu kumwokoa lakini sikuweza. Wakampiga tena. Akaanguka chini. Binti yangu alipigwa mkononi. Walimkokota mvulana huyo na kumwambia atambae. Alikuwa anatambaa huku wakimpiga kwa rungu hadi akatoka damu. Kijana alifariki na tukamwacha.”
Shirika la Habari la Reuters lilizungumza na kina mama zaidi ya 40, kama Adam, ambao walielezea jinsi watoto wao, wengi wao wavulana, waliuawa na wanamgambo wa Kikosi cha RSF karibu na Darfur Magharibi, mji mkuu wa El Geneina.
Kabila la Masalit
Familia zao zinatoka katika kabila la Masalit, ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya watu huko El Geneina hadi pale wapiganaji wa RSF walipowalazimisha kuondoka. Takriban watu nusu milioni, wengi wao wakiwa Masalit, wameondoka kwenda Chad kutokana na ghasia.
Maelfu wamekufa katika mashambulizi hayo. Waliofariki ni pamoja na wanawake na wasichana. Wanawake wa Masalit pia wameelezea kuvumilia unyanyasaji wa kijinsia mikononi mwa RSF inayotawaliwa na Waarabu na washirika wake, kama Reuters ilivyoeleza.
Mkimbizi wa Sudan, Radhia Yahia: “Tulikuja kupitia barabara ya Shukri. Mwanangu aliuawa kwenye barabara ya Shukri. Walimchinja. Tulifika kambi ya Adre miezi minne iliyopita na tumechoka.”
Masalit Wawindwa na RSF
Wanaume wa Masalit pia waliwindwa na RSF na washirika wake. Katika awamu nyingine ya ghasia huko El Geneina mapema mwezi Novemba, Reuters ilifichua kuwa mamia ya vijana wa Kimasalit walikusanywa na kupelekwa katika maeneo mbalimbali jijini humo ambapo walioshuhudia walisema baadhi yao waliuawa.
Naibu mkuu wa RSF Abdelrahim Dagalo anaeleza: “RSF haitatoa ulinzi kwa watenda maovu lakini itawashughulikia kikamilifu. Tunathibitisha utayari wetu kamili wa kushirikiana na kamati za uchunguzi na kuwakabidhi watu waliohusika na ukiukwaji wowote kwa ajili ya kesi ya haki.”
Masoud Mohammed Youssef, mratibu wa kikundi ambacho kinawakilisha baadhi ya makabila ya Waarabu huko El Geneina, aliyataja madai ya Wamasalit kuwa RSF ililenga watoto wa kiume hayakuwa na msingi.
Hata hivyo katika kukiri yale yanayoendelea Sudan, Abdullah Omar Abdullah, mwanajeshi wa jeshi la Sudan, alisema alikimbia na kundi la watu wengine 16 wa Masalit mapema mwezi Novemba.
Abdullah alikuwa ametoroka kambi yake ya jeshi huko Ardamata, wilaya iliyo nje kidogo ya El Geneina. Kambi hiyo ilikuwa imezidiwa na vikosi vya RSF huku wanajeshi hao wakiimarisha umiliki wake katika mji huo.
Mwanajeshi wa Sudan Aeleza Masikitiko Yake
Abdullahi Omar, Mwanajeshi wa Sudan anaeleza masikitiko yake:
"Kwa jina la Mungu, inasikitisha sana, inasikitisha, inasikitisha. Ukiona mwanamke amebeba mtoto mgongoni anakuja na kusema simama ili kumzuia. ‘Huyu mtoto ni mvulana au msichana?’ Anapomwona ni mvulana, wanamuua mara moja. Wanaua bila maneno zaidi."
Mtaalam wa Masuala ya Mauaji ya Kimbari
Melanie O’Brien, Profesa katika Kituo cha Mafunzo ya Masuala ya Mauaji ya Kimbari katika Chuo Kikuu cha Minnesota, ameyataja mauaji yanayoendelea Darfur kuwa ya kimbari.
Melanie O’ Brien, Profesa katika chuo cha Minnesota anaeleza:
"Uhalifu tunaoshuhudia unaofanyika Darfur mwaka huu bila shaka ni sawa na uhalifu wa mauaji ya halaiki. Uhalifu haufanyiki kwa siri na sio mara ya kwanza kutokea. Unafanyika katika muktadha wa historia ndefu ya vurugu, historia ya ghasia ambazo hapo awali ziliitwa mauaji ya halaiki. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu bado ina hati ya kukamatwa kwa rais wa zamani wa Sudan kwa uhalifu wa mauaji ya halaiki kwa muktadha huu wa uhalifu uliofanywa huko Darfur. Tunachokiona kwa sasa ni uhalifu dhidi ya jinsia, ikiwa ni pamoja na mauaji ya wavulana na wanaume wenye umri wa kuingia katika jeshi."
Umoja wa Mataifa
Data zilizokusanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, UN, nchini Chad zinaonyesha zaidi ya robo ya wakimbizi 484,000 waliokimbia Sudan mwaka huu na sasa wanaishi katika kambi ya mpakani.
Kulingana na data hizi, UN unakadiria karibu mara mbili ya wanawake watu wazima kuliko wanaume ndiyo wamevuka mpaka.
Desemba 2023, Marekani ilieleza kwamba RSF na Jeshi la Sudan wamefanya uhalifu wa kivita tangu mapigano yalipozuka na kuenea hadi Darfur.
Juhudi za kuifikia RSF kujibu baadhi ya maswali kutoka Reuters hazikufanikiwa. Katika taarifa za awali, jeshi hilo limesema halikuhusika katika kile ilichokitaja kuwa mzozo wa kikabila huko El Geneina.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Hubbah Abdi, Washington DC.