SUDAN : Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ajiuzulu, wananchi washinikiza kuundwa serikali ya kiraia

Salah Abdallah Mohamed Saleh akizungumza na vyombo vya habari Khartoum, Sudan, Julai 10, 2013, wakati akitangaza kujiuzulu Jumamosi.

Baada ya kuapishwa Mkuu mpya wa baraza la kijeshi la mpito nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Ijumaa, kiongozi huyo ameahidi kufanya mabadiliko katika taasisi za iliyokuwa serikali ya Omar al-Bashir.

Al-Burhan ameahidi kuundwa kwa serikali ya kiraia baada ya Ijumaa mkuu wa baraza la mpito la kijeshi Ahmed Awadh Auf kujiuzulu katika hotuba yake iliyorushwa mubashara kupitia televisheni ya taifa.

Burhani amewahakikishia wananchi kuwa wale wote walioshiriki katika mauaji ya waandamanaji watahukumiwa kisheria na ametangaza pia kuondoa marufuku ya kutembea usiku. Kadhalika ameamuru kuachiwa huru kwa watu wote waliowekwa kizuizini chini ya sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa na utawala ulioangushwa.

Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani imeripoti Jumamosi kuwa taarifa zaidi zinasema kuwa watu 16, wakiwamo wanajeshi, wameuawa katika siku mbili za nyuma tangu vikosi vya jeshi kumuondoa madarakano al-Bashir katikati ya maandamano ya kuipinga serikali yake ya miezi kadhaa.

Pia imeongeza kuwa Kamati ya Madaktari ya Sudan, ambayo inahusika na maandalizi ya maandamano hayo, imesema watu 13 wameuawa kwa kupigwa risasi Alhamisi, na watu wengine watatu akiwamo mwanajeshi waliuawa Ijumaa. Kamati hiyo imeelza kwamba walikufa "mikononi mwa vikosi vya utawala na wanamgambo wake."

Vyombo vya habari vimemnukuu Al-Burhan akitoa amri kuwa wafungwa wote wa kisiasa wataachiliwa huru. Burhani ameongeza kwamba serikali ya kiraia itaundwa baada ya majadiliano na upinzani katika kipindi cha mpito ambacho kitadumu kwa muda wa miaka miwili.

"Natangaza kufanya mabadiliko ya taasisi za dola kulingana na sheria na naahidi kupambana na rushwa pamoja na kuuondoa utawala ulipita," amesema Jenerali Abdel Fattah al-Burhan," amesema siku moja baada ya kuapishwa kama mkuu wa baraza jipya la kijeshi la mpito nchini Sudan.

Taarifa kutoka jeshi la Sudan zinasema kuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (NISS), Salah Mohamed Saleh alikuwa amejiuzulu. Mkuu huyo wa upelelezi ambaye anajulikana pia kama Salah Gosh, alikuwa kiongozi muhimu wa usalama chini ya uongozi wa al-Bashir.

Wakati huo huo, maelfu ya waandamanaji wamejitokeza Sudan Jumamosi, na kuelekea katika makao makuu ya Jeshi hilo mjini Khartoum, baadhi wakiwa katika magari na wengine wakitembea kwa miguu.

Hii ni kuitikia wito wa viongozi wa harakati hizi ambao walikuwa wamewataka waendeleze maandamano kwa muda mrefu na ambayo yamepelekea viongozi wawili kujiuzulu katika kipindi cha siku mbili.

Taarifa za vyombo mbalimbali vya habari nchini Sudan na ulimwenguni zinaeleza kuwa waandamanaji wa Sudan wamesema wanapanga kuendelea kumiminika barabarani hadi pale serikali ya kiraia itakapoingia madarakani.

Miezi kadhaa ya maandamano yaliyoongozwa na vyama vya wafanyakazi wa taaluma mbalimbali pamoja na asasi za kiraia yalipelekea kuondolowa madarakani kwa kiongozi wa miaka thelthini Omar al-Bashir.