Serikali ya Somalia imesema kwamba wanamgambo 43 wa al-Shabab, wakiwemo makamanda wawili waandamizi, waliuawa na vikosi vya Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNA) wakati wa shambulio la anga la mwishoni mwa wiki, takriban kilomita 14 kutoka Wilaya ya Jamame katika eneo la Lower Jubba.
"Shambulio hilo la anga lilifanikiwa kuwaangamiza viongozi wakuu wa al-Shabab Aden Abdirahman Aden na Idris Abdirahim Nur, ambaye alikuwa na asili ya Kenya, na jumla ya wapiganaji 43 wa Al-Shabab," Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia (SONNA) liliripoti Jumatatu.
SONNA ilisema shambulio hilo, lililofanywa na "washirika wa kimataifa wa Somalia," lilifanyika Ijumaa wiki jana wakati wanamgambo na makamanda wao walikusanyika kupanga mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali katika kambi ya kijeshi ya Barsanguni, ambayo ni nyumbani kwa Jeshi la Taifa la Somalia na vikosi vya ndani. Taarifa hiyo haikutaja mshirika wa kigeni aliyefanya shambulizi hilo la anga, lakini mara nyingi ndege zisizo na rubani za Kamandi ya Marekani barani Afrika, hufanya mashambulizi dhidi ya wapiganaji nchini Somalia.
"Kutatizwa kwa mafanikio yashambulio hilo lililopangwa, kunaonyesha ufanisi wa juhudi zinazoendelea za kupambana na al-Shabaab na kuwalinda watu wa Somalia," taarifa hiyo iliongeza.
Hayo yanajiri wakati ambapo nalo Baraza la Mawaziri la Somalia limemteua Brigedia Jenerali Ibrahim Sheikh Muhyadin Addow kama kamanda mpya wa Jeshi la Kitaifa la Somalia.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Somalia alisema uteuzi huo unafuatia pendekezo la kumuondoa Jenerali Odawa Yusuf, ambaye ameshikilia wadhifa huo tangu Machi 2019.