Maafisa wanane wa polisi wa Kenya waliuawa wakati gari lao lilipolipuliwa na kifaa cha kulipuka katika shambulio linaloshukiwa kufanywa na kundi la jihadi lenye makao yake nchini Somalia, la al-Shabab, polisi wamesema.
Tukio hilo lilitokea Jumanne katika kaunti ya Garissa mashariki mwa Kenya, eneo lililo mpakani na Somalia, mahala ambako al-Shabab wamekuwa wakiendesha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali tete mjini Mogadishu kwa zaidi ya miaka 15.
Tulipoteza maafisa wanane wa polisi katika shambulio hili, alisema Mkuu wa eneo la Kaskazini Mashariki, John Otieno. Tunashuku ni kazi ya al-Shabab ambao hivi sasa wanavilenga vikosi vya usalama na magari ya abiria.
Kenya kwa mara ya kwanza ilituma wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2011 kupambana na wanamgambo wenye uhusiano na al-Qaida na kwa sasa, nchi hiyo ni mchangiaji mkubwa wa wanajeshi katika operesheni ya kijeshi ya Umoja wa Afrika dhidi ya kundi hilo.
Lakini imetaabika na msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi, ikiwa ni pamoja na shambulizi lililopelekea umwagaji damu katika jengo la biashara la Westgate jijini Nairobi mwaka 2013, ambalo lilisababisha vifo vya watu 67, na shambulio katika Chuo Kikuu cha Garissa mwaka 2015 ambalo liliua watu 148.
Forum