Shirika la habari la ROITA halikuweza kuthibitisha haraka taarifa zinazokuja kutoka mji wa Kramatorsk.
Gavana wa Donetsk, Pavlo Kyrylenko amesema maelfu ya raia wamekuwepo katika kituo hicho wakati roketi zilipopiga, katika kile alichokieleza kuwa ni shambulizi la makusudi.
Amesema wengi wa waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Wizara ya ulinzi ya Russia ilinukuliwa na shirika la habari la RIA ikisema kuwa makombora yanayosemekana kupiga kituo hicho yalikuwa yakitumiwa na jeshi la Ukraine tu na kwamba vikosi vya Russia havikupangwa kulenga Kramatorsk ijumaa.
Kwa upande wake rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema hakuna wanajeshi wa Ukraine waliokuwepo katika kituo hicho.
Moscow imekanusha kuwalenga raia tangu ilipovamia Ukraine February 24 kwa kile inachokiita ni operesheni maalumu za kijeshi.
Leo Umoja wa Ulaya umeidhinisha sehemu ya nne ya vikwazo dhidi ya Russia tangu uvamizi huo ulipoanza ikiwemo marufuku ya ununuzi wa makaa ya mawe, mbao, kemikali na bidhaa nyingine.