Sanamu ya Desmond Tutu yenye kitambaa cha Kipalestina kuwekwa katika maonyesho Cape Town

Desmond Tutu alipokuwa akizungumzia suala la Waisraeli na Wapalestina kufanya Amani ya kudumu. Picha na REUTERS/Jim Hollander

Sanamu ya Askofu wa Afrika Kusini Desmond Tutu akiwa amevalishwa kitambaa cha Palestina shingoni itawekwa katika jiji la Cape Town siku ya Ijumaa ikiwa ni ishara ya miongo mingi ya utetezi wake wa haki za Wapalestina, taasisi yake imesema.

“Sanamu kubwa” ya mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel aliyefariki, itakuwa katika maonyesho ya muda “mpaka mashambulizi ya mabomu huko Gaza yatakaposimama” Taasisi ya urithi ya Desmond na Leah Tutu imesema siku ya Alhamisi.

“Alikuwa mkosoaji wa sera za Israel kwa Palestina na Wapalestina, ambazo alizifananisha na sera na vitendo vya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini,” taasisi hiyo ilisema.

Wakati huo huo katika mji wa Cape Town darzeni ya watu wameingia mitaani siku ya Alhamisi ikiwa ni moja ya maandamano kadhaa yaliyopangwa kufanyika kote nchini Afrika Kusini kuiunga mkono serikali kwa kuwasilisha kesi ya ‘mauaji ya kimbari’ dhidi ya Israel.

Waandamanaji wakiwa nje ya mahakama kuu huko Afrika Kusini.

Wanasheria wa Pretoria wanawasilisha kesi yao katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataia huko The Hague, ambako Afrika Kusini imewasilisha ombi la dharura kutiaka mahakama kuilazimisha Israel “kusimamisha haraka” operesheni zake za kijeshi huko Gaza.

Wakiwa wamesimama katika ngazi za Mahakama Kuu iliyoko kusini magharibi katika mji wa bandari wa Cape Town, waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina walibeba mabango yanayosomeka “acha mauaji ya kimbari” na “Susia ubaguzi wa Israel”

Baadhi yao wakiimba “iachie huru Palestina”

Suala muhimu kwetu ni kwamba kuwepo kwa sitisho la vita, vitendo vya kijeshi visimaishwe huko Gaza,” alisema Seehaam Samaai, mwanasheria aliyehudhuria maandamano hayo.

Maandamano zaidi yamepangwa kufanyika Cape Town na miji mingine.

Afrika Kusini inadai kuwa Israel inavunja ahadi zake chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mauaji ya kimbari, ikidai mashambulizi ya mabomu na uvamizi wa Gaza “una nia ya kufanya uharibifu kwa kiasi kikubwa kwa utaifa wa Palestina, rangi na ukabila.”

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP