Russia yadai uhusiano wake na Marekani si mzuri

Rais wa Russia Vladimir Putin akizungumza na msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov huko Astana, Kazakhstan Novemba 27, 2024. Picha na REUTERS

Rais wa Russia Vladimir Putin akizungumza na msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov huko Astana, Kazakhstan Novemba 27, 2024. Picha na REUTERS

Russia imesema kwamba uhusiano wake na Marekani ni mbaya kiasi kwamba raia wake wameshauriwa kutosafiri kwenda Marekani, Canada au baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya kwa sababu wanakabiliwa na hatari ya kuandamwa na mamlaka za Marekani.

Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova, amesema uhusiano wa Russia na Marekani uko katika hali ya kuvunjika kabisa.

Wanadiplomasia wa Russia na Marekani wanasema uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni mbaya kuliko ilivyokuwa wakati wa mgogoro wa makombora ya Cuba mwaka 1962.

Uhusiano umeharibika kutokana na uvamizi wa Russia nchini Ukraine, na ulifikia kiwango kibaya zaidi mwezi uliopita baada ya Ukraine kuanza kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani na Uingereza kutekeleza mashambulizi ndani ya Russia na kupelekea Russia kufanyia marekebisho sheria zake za matumizi ya silaha za nyuklia.