Mahakama moja nchini Ufaransa imemhukumu Rais wa zamani Nicolas Sarkozy kutumikia kifungo cha mwaka moja jela baada ya kumkuta na hatia ya matumizi ya fedha za kampeni kinyume cha sheria wakati wa kampeni yake mwaka 2012 kutaka kuchaguliwa tena.
Waendesha mashtaka wanasema Sarkozy alitumia karibu mara mbili ya kiwango kilichoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Ufaransa katika uchaguzi ambao hasimu wake Francois Hollande alishinda.
Sarkozy, ambaye aliiongoza Ufaransa kuanzia mwaka 2007-2012, amekataa kufanya kosa. Wakili wake amesema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama.
Mahakama hiyo imesema anaweza kutumikia kifungo chake nyumbani huku akivaa bangili ya elektroniki ya kumfuatilia.
Sarkozy alikutwa na hatia kwa makosa ya rushwa katika kesi ynyingine mwezi Machi, na alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela huku miaka miwili ikisitishwa. Amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.