Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema serikali yake inafanya juhudi kubwa kurejesha amani nchini baada ya shambulio kali la wanamgambo mwezi Machi, 2021.
Wanamgambo wa kikundi cha Kiislam walishambulia na kuuwa raia karibu na miradi ya gesi ya mabilioni ya dola katika mji wa Palma.
"Tutafanya juhudi zote kurudisha amani katika nchi yetu, hasusan upande wa kaskazini, huko Cabo Delgado ambako katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa shabaha ya mashambulio ya kigaidi," Rais alisema.
Ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa wadau wa Madini ya Nishati, Nishati, Mafuta na Gesi ya Msumbiji mjini Maputo.
Wanamgambo walishambulia mji wa pwani wa Palma mnamo Machi 24, katika wilaya karibu na vinu vya gesi asili, ambayo wachambuzi wanasema, inaweza kubadilisha hali ya uchumi wa Msumbiji.