Rais Kenyatta atangaza maombolezo ya kitaifa kumuenzi hayati Kibaki

Rais wa zamani Mwai Kibaki Nairobi, Kenya, April 9, 2013.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza kipindi cha maombolezo kitaifa na bendera kupepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza kipindi cha maombolezo kitaifa na bendera kupepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki.

“ Kama kiongozi mkuu katika historia ya kenya baada ya uhuru , Mwai Kibaki alipata heshima na mapenzi makubwa ya watu wa taifa hili na mataifa mengine duniani kote.

“Rais Kibaki atakumbukwa daima kama mwanasiasa muungwana wa kenya , mtoa mada mahiri ambaye ufasaha, na haiba yake vilishinda daima,”ameeleza Rais Kenyatta.

Rais Uhuru Kenyatta. REUTERS/Monicah Mwangi

Baada ya kuondoka madarakani mwaka 2013 , kibaki alijihusisha kwa mara chache katika maisha ya umma.

Alianza kuugua mwaka 2016 na maafisa wa serikali na familia yake hawakuwa wakitoa taarifa za afya yake.

Alifurahia maisha mazuri ya afya yake wakati mwingi wa maisha ya utu uzima, akijulikana kuwa mcheza golf wa kudumu nchini humo hadi alipojeruhiwa katika ajali ya barabarani mwaka 2002.

Kibaki amelitumikia taifa la Kenya kama rais wa tatu kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2002-2013 na kama mbunge kwa miaka 50 mwaka 1963-2013.

Pia alishika nyadhifa mbali mbali za uongozi katika serikali wakati wa rais wa kwanza wa taifa hilo Jomo Kenyatta na baadaye katika uongozi wa enzi ya Daniel Arap Moi.

Alipojiunga na bunge mwaka 1963 Kibaki aliteuliwa na hayati Rais Jomo Kenyatta kama katibu mkuu wa Hazina na mwaka 1966 akawa waziri msaidizi wa fedha na mwenyekiti wa tume ya mipango ya uchumi.

Baadae aliongoza wizara za biashara na viwanda na fedha na mipango ya uchumi.

Kibaki pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa kenya kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1978 -1988 chini ya utawala wa Moi aliyefariki February mwaka 2020.

Aliacha nafasi hiyo baada ya kutofautiana na Moi na kuwa mbunge wa upinzani kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 2002, alipochaguliwa kuwa rais wa tatu baada ya majaribio mawili bila mafanikio mwaka 1992 na mwaka 1997.