Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 21:33

Viongozi wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, wamejadili M23


Wanajeshi wa DRC wakishika doria mashariki mwa Congo baada ya kuwafurusha waasi wa M23 katika sehemu za Bunagana, Rwanguba na Kabinti, wilayani Rutshuru. April 2022. PICHA: Austere Malivika
Wanajeshi wa DRC wakishika doria mashariki mwa Congo baada ya kuwafurusha waasi wa M23 katika sehemu za Bunagana, Rwanguba na Kabinti, wilayani Rutshuru. April 2022. PICHA: Austere Malivika

Viongozi wa Kenya, Uganda, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi, wamekutana Nairobi, na kujadiliana kuhusu mapigano yanayoendelea kati ya makundi ya waasi na wanajeshi wa serikali ya congo.

Mapigano ya kundi la M23 yanaendelea mashariki mwa DRC karibu na Uganda.

Viongozi wa nchi hizo wamejadili jinsi ya kurejesha utulivu katika maeneo yanayokabiliwa na vita na kuweka mkakati wa kuafikia muafaka wa kuleta usalama nchini DRC.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ameongoza kikao cha Rais Felix Antoine-Tsisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Evariste Ndayishimiye wa Burundi na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pamoja na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Rwanda aliyemwakilisha rais Paul Kagame.

Mapigano ya M23

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kwa muda sasa kati ya jeshi la DRC, FARDC na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.

Mkutano huo ni muendelezo wa mkutano mdogo uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Nairobi uliowaleta pamoja viongozi wa kanda ya nchi za Maziwa Makuu kujadili hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Miongoni mwa yaliojadiliwa na marais hawa ni kuzuka upya kwa waasi wa M23 na makundi mengine yenye silaha kali, ndani na nje ya DRC ambayo bado yamejificha mashariki mwa nchi hiyo kama kundi la allied democratoc forces – ADF, Mai mai, Codeco, na kuendelea kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali.

Waasi wa M23 walikuwa wametangaza kusitisha mapigano wiki iliyopita, baada ya makabiliano mabaya mashariki mwa DRC ambapo watu kadhaa na wanajeshi waliuawa huku maelfu ya watu wakikimbilia Uganda.

Wakati huo msemaji wa kundi hilo Willy Ngoma aliambia idhaa ya kiswahili ya sauti ya Amerika kwamba walikuwa wamesitisha vita ili kuruhusu fursa ya kufanyika mazungumzo kati yao na serikali ya DRC.

Ushirikiano wa jeshi la DRC na la Uganda

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC, limekuwa na mpango wa kushambulia sehemu walipo wapiganaji wa M23, kusini mashariki mwa DRC, wakati jeshi la Uganda likionekana kuimarisha usalama katika mpaka wake hasa eneo la Bunagana, ili kudhibiti mapigano kusambaa hadi nchini Uganda.

Mkutano wa baadhi ya viongozi wa Afrika mashariki unajiri wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeishtumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi hao wa M23, madai ambayo yamepingwa na Rwanda.

Maoni ya wachambuzi

Mchambuzi wa maswala ya diplomasia Prof Chacha Nyaigoti Chacha, ameambia Sauti ya Amerika kwamba Kenya ni “muhimu katika kutatua vita vya DRC kwa sababu haijajihusisha moja kwa moja katika mgogoro huo. Kuwepo kwa mkutano huu nchini Kenya chini ya rais Uhuru Kenyatta ni thibithisho tu kwamba wote wamekubali kwamba wanaweza kusikilizana.”

Haijabaibika iwapo waasi wa M23 ni sehemu ya mazungumzo haya lakini Professa Chacha anaeleza kuwa ndiposa pawepo na suluhu ya kudumu, wanahitajika kuwa sehemu ya mazungumzo hayo, ambayo yamefanywa kisiri jijini Nairobi.

“Nafikiri wakiwa sehemu ya mazungumzo hayo, wataelezwa makubaliano yaliyopatikana na kuambiwa kile wanachotakiwa kutekeleza kwa sababu wao ndio chanzo cha matatizo yanayojadiliwa kwa sasa.” Amesema Profesa Chacha Nyaigoti Chacha.

Mapigano kati ya kundi la M23 na jeshi la DRC, yameathiri maeneo mengi kama vile Kinyamahura, Jomba, Kanombe, Runyoni, na kusambaa katika vijiji kadhaa vya mkoa wa Rutshuru, Kivu Kaskazini.

Kwa upande mwingine, Jeshi la DRC kwa ushirikiano na jeshi la Uganda la UPDF linapambana na waasi wanaoaminika kutoka Uganda wa allied democratic forces, ADF katika wilaya ya Ituri na Beni.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG