Polisi Korea Kusini watuma maafisa wa upekuzi katika ofisi ya rais wa nchi hiyo

Waandamanaji wakiwa katika maandamano ya kumtaka rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol ashtakiwe. Picha na Reuters

Polisi nchini Korea Kusini wamesema wamepeleka maafisa kufanya upekuzi katika ofisi ya rais Yoon Suk Yeol leo Jumatano, kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea baada ya kutangaza matumizi ya sheria ya kijeshi.

Haijabainika iwapo upekuzi huo umeanza.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kwamba walinzi wa rais hawawezi kuwaruhusu polisi kupekua ofisi yake kutokana na sheria inayozuia uchunguzi kufanyika katika ofisi zenye siri za serikali bila idhini ya maafisa wanaosimamia ofisi hizo.

Yoon aliomba msamaha Jumamosi, kutokana na hatua yake ya kutangaza matumizi ya sheria ya kijeshi na kusema kwamba hatakwepa uwajibikaji wa kisiasa au kisheria.

Kiongozi wa chama tawala cha Yoon, baadaye aliapa kuwa ataandaa mpango madhubuti kwa rais huyo kuondoka madarakani kwa utulivu.

Maoni hayo yalikosolewa kuwa hayana msingi na kinyume cha katiba lakini yamesababisha maswali mengi kuhusu anayeiongoza Korea kusini na jeshi lake, wakati kuna mviutano mikubwa na Korea kaskazini.