Polisi Addis Ababa wapambana na waamini nje ya Msikiti

የኢትዮጵያ ካርታ

Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kwa waumini siku ya Ijumaa nje ya msikiti mkubwa kuliko yote ulioko nje ya jiji la Addis Ababa, katika mapigano ya hivi karibuni ambayo yalichochewa na uharibifu wa misikiti katika mji mkuu huo wa Ethiopia.

Maeneo kadhaa ya ibada ya Waislamu yameharibiwa mjini Addis Ababa katika miezi ya hivi karibuni, uharibifu huo ni sehemu ya mradi wenye utata wa mipango miji ambao umezua hasira miongoni mwa waumini.

Ijumaa iliyopita, mapigano yalizuka nje ya Msikiti wa Grand Anwar, na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine dazeni kujeruhiwa, polisi ilisema na kwamba waliwakamata watu 114.

Kabla ya sala ya Ijumaa ya wiki hii, waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP waliwaona polisi wakiwa wamevalia zana za kutuliza ghasia wakiwa nje ya msikiti huo.

Wajumbe wa Republican Guard, kitengo chenye jukumu la kulinda taasisi na maafisa wa serikali, pia walikuwepo.

Waumini walikuwa wakitoka msikitini kwa utulivu wakati baadhi ya vijana walipo anza kupiga kelele "Allahu Akbar" na milio ya risasi ilianza kusikika, na kusababisha hofu, waandishi wa habari wa shirika la AFP waliona.

Baadhi ya watu waliokuwemo katika umati huo waliwarushia mawe polisi, na polisi waliwajibu kwa mabomu ya kutoa machozi.

Haijajulikana kama polisi walitumia risasi, makombora ya plastiki au au walipiga risasi tupu.

Milio ya risasi iliendelea kusikika kwa takriban saa mbili kabla ya hali ya utulivu kurejea, huku polisi wakiwa wamezingira barabara zilizopo jirani na msikiti huo.

Amir, muumini na kijana aliyekuwepo katika msikiti huo wakati wa sala ya Ijumaa alisema: "Tulifahamu kiasi kitakachotokea baada ya swala." "Mamia ya kaka na dada zetu walikamatwa wiki iliyopita... watu wana hasira misikiti yetu inaharibiwa."

Mradi wa mipango miji, unaojulikana kama Sheger City, unahusisha muunganisho wa manispaa kadhaa katika eneo la Oromia nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo.

Pia Mradi huo umesababisha ubomoaji wa nyumba na maeneo ya biashara, na wanaharakati wa haki za watu wa eneo hilo wameuita mradi huo kuwa ni "kinyume cha sheria "

Chanzo cha bahari hii ni Shirika la habari AFP.