Papa Francis atoa wito wa msaada wa dharura kwa Somalia

Papa Francis

Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, Jumapili alitoa wito wa msaada wa kimataifa kwa Somalia, ili kusaidia nchi hiyo kukabiliana na ukame, aliosema unasababisha maafa, na  ambao Umoja wa Mataifa unasema umewaacha takribana watu milioni moja  bila ya makazi.

Papa Francis ameiita hali hiyo kuwa "mgogoro mkubwa wa kibinadamu" ambao hauathiri tu Somalia, mbali pia nchi jirani katika eneo hilo. Kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 85 ameyasema hayo hii leo baada ya ibada yake ya kila Jumapili, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Somalia na majirani zake katika Pembe ya Afrika, Ethiopia na Kenya zimekumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, ulitokana na ukosefu wa mvua ya kutosha kwa vipindi vine, kwa mujibu wa mashirika ya hisani.

Umoja wa mataifa umesema hali hiyo imeathiri mazao na mifugo. Shirika la Umoja wa Matiafa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR limesema kupitia taarifa iliyotolewa Alhamisi kwamba zaidi ya watu 755,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Somalia, na kwamba idadi hiyo ikijumuishwa na wale walivuka mipaka na kuingia katika nchi jirani, inafikia takriban milioni moja.